January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wataalamu wa afya wapewa somo

Na Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma

MKUU wa Wilaya ya Dodoma Mjini,Jabir Shekimweli amesema Madaktari, Wauguzi na Watumishi wa sekta ya afya kwa ujumla wanayo majukumu ambayo yanawataka kuzingatia haki za binadamu na utawala bora katika utoaji wa huduma na kuhamasisha utekelezaji wa haki ya afya na misingi ya utawala bora nchini.

Shekimweli amesema hayo jijini wakati akifungua mafunzo ya haki na utawala bora kwa watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo ambapo amesema,lengo kuu la mafunzo hayo ni kuongeza uelewa kwa watumishi wa sekta ya afya kuzitambua, kuzielewa na kuzijua haki za binadamu na misingi ya utawala bora ili iwasaidie kufanya kazi zao za kila siku hasa utoaji wa huduma za afya kwa kuzingatia viwango vya haki za binadamu na misingi ya utawala bora.

“Inatarajiwa kuwa elimu hii itawasaidia watumishi kujenga utamaduni wa kuheshimu, kutetea, kukuza na kulinda haki za binadamu pamoja na misingi ya utawala bora katika maeneo yao ya kazi na hii itawawezesha pia kuelimisha wagonjwa mifumo sahihi ya kufuata na kuweza kupata huduma za afya kwa haraka na wepesi zaidi,”amesema

Amesema, watumishi wa afya ni sehemu muhimu katika kuhakikisha jamii ambayo wananchi hawasumbuliwi na magonjwa na upatikanaji wa hivyo kutoa mwanya wa kushiriki ipasavyo katika shughuli za uchumi na maendeleo.

“Na kwa kutambua mchango huu muhimu wa sekta ya afya katika ustawi na maendeleo ya nchi Serikali inaendelea kuboresha na kuimarisha hali ya huduma za afya nchini kwa kuongeza miundombinu, vifaa, watoa huduma ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya utendaji kazi na msalahi yao,”amesema.

Aidha, amesema uwajibikaji wenye kuzingatia utaalam, sheria, kanuni, na miongozo ndio msingi kwa sekta ya afya katika kutoa huduma bora inayokidhi mahitaji.

“Elimu hii ya Haki za binadamu na Utawala bora mtakayoipata kwa siku tatu, iwe na nafasi kwa kila mmoja kujitathmini kiutendaji, pia kuchukua hatua za kukabiliana na changamoto zinazokwamisha utoaji wa huduma bora ya afya kwa mfano rushwa, kutoa huduma zisizokidhi matarajio ya wananchi na hivyo kusababisha malalamiko ya wananchi kwa uongozi wa hospitali na Serikali kwa ujumla,”amesema.

Pamoja na hayo amesema Katika utekelezaji wa haki za binadamu Serikali ina wajibu wa kutimiza haki yaani kuweka miundombinu, sheria, kanuni, sera pamoja na mipango ya muda mfupi na mrefu kwa nia ya kuhakikisha na kuwezesha utekelezaji na upatikanaji wa haki ya afya nchini.

Kwa upande wake Kamishna wa Tume ya hiyo, Dkt.Fatma Khalfan akizungumaza Katika Mafunzo hayo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, amesema mafunzo hayo inafungua mlango wa mashirikiano kati ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na Tume.

Amesema, katika mafunzo hayo ya siku tatu Mada za Utawala Bora na Uhusiano wake na Haki za Binadamu na Utoaji wa Huduma katika Sekta ya Afya zitatolewa na Maafisa wa Tume na Washiriki watapata fursa ya kuzifahamu na kuzijadili.

“Lengo hasa la kuandaa na kuwasilisha mafunzo haya kwa watumishi wa sekta ya afya ni kuwawezesha kuitambua, kuielewa, kuijua na kuiishi Misingi ya Utawala Bora na pia haki za Binadamu na chimbuko lake na kutumia mafunzo haya katika kuleta ufanisi na tija katika utoaji wa huduma ya afya,”amesema.

Pia amesema mafunzo haya ni kutambua mchango muhimu wa sekta ya afya katika kuhamisisha na kudumisha haki za binadamu nchini, hususani haki ya afya na majukumu ya sekta ya afya yanaendana moja kwa moja na haki za binadamu na misingi ya utawala bora,hivyo ni muhimu kufahamishana na kukumbushana wajibu huo.

“Tume imeandaa mafunzo juu ya haki za binadamu na utawala bora kwa ajili ya watumishi wa Sekta ya afya katika mikoa iliyo na Ofisi zake kote Tanzania Bara na Zanzibar, Ofisi hizo ni pamoja na Makao Makuu Dodoma na ofisi ya Zanzibar iliyoko kisiwani Unguja pamoja na matawi yake yaliyoko Dar-es-Salaam, Mwanza, Lindi na Pemba,”amesema.

Ametaja vipengele vitakavyowasilishwa kwa washiriki ni dhana ya utawala bora, misingi ya utawala bora, uhusiano kati ya utawala bora na haki za binadamu, umuhimu na uhusiano kati ya utawala bora na utoaji wa huduma ya afya na changamoto zinazokabili utawala bora.