November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

wasimamizi wa mitihani darasa la Saba waonywa

Na Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Rukwa

Mkuu wa wilaya ya Kalambo Mkaoani Rukwa Lazaro Komba amesema Wanafunzi 7,522 kati yao wavulana wakiwa 3,404 na wasichana 4,118 wanatarajia kuanza kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi wilayani Kalambo na kuwaonya vikali wasimamizi watakao bainika kuvujisha mitihani na kwamba sheria kali zitachukuliwa dhidi yao.

Aidha Komba amesema mitihani hiyo itafanyika kwenye vituo 330 kupitia shule 98 za wilaya hiyo na kila mkondo utakuwa na idadi ya watahiniwa 25 na kuwaonya vikali wazazi na walezi watakao bainika kujihusisha na tabia za kuwalaghai watoto wao kwa kuwazuia kufanya vizuri mitihani yao kwa nia ya kuwa ozesha na kwamba sheria kali  zitachukuliwa dhidi yao

Hata hivyo kwa mujibu wa afisa elimu mkoa wa Rukwa  Samson Hango ,amesema idadi ya watahiniwa kwa mwaka 2023 ni 32,217 ambapo imepungua kwa jumla ya watahiniwa 1,227 sawa na asilimia 3.8% ikilinganishwa na watahiniwa 33,444 waliosajiliwa mwaka 2022.

Amesema kuwa kwa upande wao kama serikali wameshafanya maandalizi ya kutosha na kuwa upo uhakika mkubwa wa mtihani huo kufanyika kwa usalama na kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa.

Mmoja wa  Watahiniwa hao ambaye ni mwanafunzi  wa shule ya msingi Matai B Suzana Athanas amedai kuwa na wao kama Wanafunzi wamejiandaa vyema kama walivyoandaliwa na Waalimu wao kwa kufanya mazoezi mengi na kuwahakikishia Wazazi wao kuwa watafanya vizuri kwenye mitihani yao.

Wamesema kuwa umekuwepo utaratibu wa baadhi ya Wazazi kuwaeleza Watoto wao wasifanye vizuri kwenye mitihani yao na kuwa hilo sasa halina nafasi kwa maana kila mmoja sasa anajitambua na hakuna yeyote aliye tayari kutii maagizo kama hayo.

“umekuwepo utaratibu wa baadhi ya Wazazi kutoa maelekezo kwa Watoto wao wafanye vibaya kwenye mitihani ili wafeli na wasiendelee na masomo kwa lengo la kuwaozesha na wengine kuchunga ng’ombe lakini kila mmoja amejengewa uwezo wa kukataa kutii maagizo kama hayo yanayokwenda kinyume na sheria kwani elimu ni haki yao”alisema

mtihani wa darasa la saba mwaka huu wa 2023 utafanyika Septemba 13 na 14

Mkuu wa wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa Razaro Komba
Wanafunzi wa darasa la saba shule ya msingi Matai ” B” wakiwa kwenye maandalizi ya mtihani wa darasa la saba