January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Washindi ligi ya Mpanda,Wanahabari kupelekwa kutalii hifadhi ya Katavi

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline, Mpanda.

LIGI ya mpira wa miguu ngazi ya wilaya imehitimishwa katika uwanja wa CCM Azimio manispaa ya Mpanda mkoani Katavi kwa fainali kati ya Masofa Fc dhidi ya Magamba FC zote za wilaya ya Mpanda.

Ligi hiyo iliyodhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi ilianza kuchezwa Juni, 2024 na kuhitimishwa August 20, 2024 ambapo Masofa Fc wameibuka mshindi wa michuano hiyo.

Sebastian Kapufi akizungumza kuhusu udhamini wake kwenye michezo amesema kuwa licha ya mshindi wa kwanza kupatikana na kupewa taji na fedha Tsh 500,000/- lakini wote na mashindi wa pili watapelekwa kufanya utalii hifadhini.

“Nimekuwa nikidhamini ligi ya mkoa wa Katavi zaidi ya miaka mitatu hapa suala hili sio geni nimewahi kutoa zawadi za pikipiki na zingine nyingi…ninachotaka kuwaahidi na kwa kuanzia na fainali hii mwanzo ili kuwa tutoe zawadi ya kwa mashidi wa kwanza Tsh 500,000/- wa pili Tsh 250,000/- na watatu Tsh 100,000/-“Amesema Kapufi.

“Nikawaambia tuongeze zawadi kwa mfugaji bora, golikipa bora na seti bora ya waamuzi wote hao tunawapa zawadi lakini kwa ajili ya kufurahisha mashidano hayo kwa mshindi wa kwanza na wapili ninawapeleka kutalii Katavi bila kusahau na wanahabari”amesema.

Aidha amesema katika kutambua umuhimu wa michezo wa mpira wa miguu kwa wanawake timu ambazo zimecheza kwa mchezo awali kati ya Soko Kuu Mpanda  dhidi ya Mpanda Hotel amezipatia kila moja Tsh 100,000/- kama motisha kwao.

Amesema michezo ni sekta muhimu sana katika kuchochea ukuaji wa utalii nchini akiwa mbunge anasababu ya kuhakikisha wanamichezo wanakuwa sehemu ya kushiriki sio kukuza utalii pekee bali wanaweza kuona vivutio vya nchi yao.

Kuhusu changamoto za vifaa vya mchezo ameahidi kulishughulikia “ Nitakapo kwenda Dodoma na nikirudi nitakuja na vifaa vyote ili kuhakikisha michezo inaendelea” amesisitiza.

Mratibu wa mashindano ya mpira wa miguu ngazi ya wilaya, Hassan Korongo amesema kuwa mashindano hayo yalianza kufanyika mwenzi wa sita mwaka huu yakihusisha timu 16 kwa mfumo wa makundi.

Korongo amemshukuru mbunge kwa kukubali kuwa mdhamini wa mashindano hayo kwa msimu wa 2024/2025 na kuwaomba wadau wengine kujitokeza kwaajili ya kuunga mkono sekta ya michezo hususani Mpira wa Miguu.