November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Washauriwa kuwaendeleza kielimu waliohifadhi quran

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online. Zanzibar

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amewataka wazee na walimu wa madrasa nchini kuwaendeleza kielimu katika fani mbalimbali za dini na dunia, wanafunzi waliohifadhi quran ili kupata radhi zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu.

Ameyasema hayo katika hafla ya mashindano makuu ya kuhifadhi quran ya kitaifa Zanzibar ya juzuu 30 yaliyohitimishwa katika Masjid Jaamiu Zinjibaar, Mazizini Zanzibar.

Makamu huyo wa Pili, amesema wanafunzi waliopata fursa ya kuhifadhi quran ni vyema kuandaliwa mazingira mazuri ya kielimu, ili wasiishie kushiriki mashindanoni na kupata zawadi bali waandaliwe mfumo mzuri wa kuendelea na masomo, akitolea mfano kujua tafsiri ya kile walichokihifadhi.

Ameipongeza Jumuiya ya Kuhifadhisha Quran Zanzibar kwa juhudi wanazochukua za kuwahifadhisha wanafunzi kitabu hicho kitukufu, hadi kuandaa mashindano makubwa kila mwaka ambapo alisema juhudi hizo zimefikiwa kutokana na uongozi mzuri waliyonao ndani ya jumuiya hiyo.

Pia ameipongeza Jumuiya hiyo kwa hatua nzuri iliyofikia na kutia moyo kwa kuona kuwa hadi, sasa jumuiya hiyo imeshahifadhisha zaidi ya wanafunzi 300 juzuu 30 wa jinsia zote ambapo alisema, huo ni mfano tosha kupata jamii iliyoshikamana na kitabu cha Mungu.

“Jumuiya imefanya kazi kubwa na ya kujitolea tokea ilipoasisiwa kwake, kitendo kinachoipa serikali kuangalia namna ya kuunga mkono jitihada hizo,” amesisitiza.

Ameuahidi uongozi wa Jumuiya hiyo kwamba, serikali iko tayari kuwashawishi waumini wenye uwezo kutafuta njia ya kutanzua baadhi ya changamoto zinazoikabili taasisi hiyo, likiwemo suala zima la jengo la ofisi yao.

Awali akitoa taarifa ya Jumuiya hiyo Mwenyekiti wa taasisi hiyo ya Kislamu, Shekhe Suleiman Omar ‘Maalim Sule’ amesema Jumuiya yake iliyoasisiwa mwaka 1992 hivi sasa imeshatimiza miaka 28.

Katika mashindano hayo ya kila mwaka yanashirikisha wanafunzi kutoka mataifa ya Afrika Mashariki, ambapo mwaka huu yamejumuisha wanafunzi wa Zanzibar pekee kwa kuhifadhi juzuu 30, yaliyoanza mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan.