January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Baadhi ya viongozi wakuu wa Vyama Vikuu vya Ushirika katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Magharibi wakimsikiliza mgeni rasmi (hayupo pichani) kwenye uzinduzi rasmi wa Umoja huo uliofanyika Makao Makuu ya Chama Cha Ushirika Mkoani Shinyanga - SHIRECU (1984) Ltd. Picha na Suleiman Abeid

Wapongeza kuanzishwa umoja wa vyama vya ushirika zao la pamba

Na Suleiman Abeid,TimesMajira Online,Shinyanga

BAADHI ya wakulima wa zao la pamba katika wilaya za Kishapu na Shinyanga wamewapongeza viongozi wa Vyama vikuu 11 vya Ushirikal katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Magharibi kwa kuanzisha umoja wenye lengo la kuwakomboa wakulima wa zao hilo.

Baadhi ya viongozi wakuu wa Vyama Vikuu vya Ushirika katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Magharibi wakimsikiliza mgeni rasmi (hayupo pichani) kwenye uzinduzi rasmi wa Umoja huo uliofanyika Makao Makuu ya Chama Cha Ushirika Mkoani Shinyanga – SHIRECU (1984) Ltd. Picha na Suleiman Abeid

Wakizungumza na waandishi wa habari juzi mjini Shinyanga wakulima hao walisema umoja wa vyama vya ushirika ulioanzishwa utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza kama siyo kumaliza kabisa changamoto za muda mrefu zinazowakabili wakulima wa zao la pamba nchini.

Mmoja wa wakulima hao, Sylvester Maganga mkazi wa kijiji cha Ngofila wilaya Kishapu amesema moja ya mambo wanayoyategemea ni upatikanaji wa pembejeo za kilimo na viuatilifu kwa bei nafuu na kwa wakati ikilinganishwa na hivi sasa ambapo mara nyingi makampuni ya ununuzi wa pamba ndiyo huwasambazia pembejeo.

“Kuanzishwa kwa umoja huu ni ukombozi kwetu sisi wakulima wa zao la pamba, tunaamini zile changamoto tulizokuwa tukipambana nazo hivi sasa zitapungua kwa kiasi kikubwa, na hata suala la bei ya viuatilifu na pembejeo nyingine tutazipata kwa bei nafuu, tunawapongeza waliobuni muungano huu,” ameeleza Maganga.

Mkulima mwingine mkazi wa kijiji cha Ngulu kata ya Ngogwa wilayani Kahama, Samson Charles alisema moja ya mambo wanayoyatarajia kutokana na umoja ulioanzishwa ni kupatikana kwa bei nzuri ya pamba kwa vile umoja huo unaweza kujitafutia wenyewe masoko ya uhakika badala ya kutegemea wanunuzi binafsi.

“Tunaupokea umoja huu, iwapo watasimama kidete suala la kupata bei ndogo ya pamba litamalizika, naamini viongozi watatafuta masoko yenye bei nzuri, mfano mwaka huu, tumejionea kwa Chama cha Ushirika Kahama, (KACU) na Chato (CCU) wamenunua kwa zaidi ya shilingi 900 kwa kilo moja badala ya shilingi 810.00,” alieleza Charles.

Katika hatua nyingine Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Mara (PMCU) ambacho ni miongoni mwa vyama 11 vilivyoanzisha umoja huo kimeiomba Serikali iangalie uwezekano wa kukipatia kiwanda kimoja cha kuchambua pamba ili kuweza kuongeza ufanisi na kuwa na ushirika wenye nguvu.

Katika taarifa yake mwakilishi wa Meneja mkuu wa PMCU, Neema Stiven alisema iwapo chama chao kitapatiwa kiwanda cha kuchambua pamba kitaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuwakwamua wakulima wa zao la pamba mkoani Mara kutoka kwenye janga la umaskini.

“Tunatarajia kukabidhiwa kiwanda cha Mugango Ginnery na Mfilisi wa iliyokuwa Mara Co operative Ltd. (MCU) tunaamini kitatuwezesha kufanya kazi zetu kwa ufanisi mkubwa lakini pia tutaongeza ajira kwa wakazi wa mkoa wetu, na tutajenga ushirika wenye nguvu hasa ikizingatiwa tumo kwenye umoja wa vyama vikuu 11 vya ushirika vilivyoanzishwa,”

“Kupitia umoja huu tutajitahidi kujenga ushirika wenye nguvu ili kuweza kutekeleza kwa vitendo adhima ya Serikali yetu ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ambaye ameonesha nia ya dhati ya kufufua ushirika hapa nchini na sisi wana Mara kwa sauti moja tunamuunga mkono kwa dhati,” ameeleza Neema.

Vyama vianzilishi vya umoja huo ni kutoka mikoa ya Mwanza (NCU), Shinyanga (SHIRECU) na Kahama (KACU), Simiyu (SIMCU), Geita (GCU) na Chato (CCU) Mara (PMCU), Tabora (IGEMBENSABO), Katavi (LATCU), Singida (SIFACU), Mbogwe/Bukombe (MBCU) na kile cha Singida/Manyoni (CEAMCU).