November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wapewa siku saba kusaka wanafunzi wasioripoti sekondari Singida

Na Jumbe Ismailly,TimesMajira online,Igunga

SERIKALI wilayani Igunga,mkoani Tabora imetoa muda wa siku saba kwa maafisa watendaji wa kata zote 35 za wilaya hiyo kuhakikisha wanawasaka kwa hali na mali wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwaka 2021 ambao mpaka sasa bado hawajaripoti katika shule walizopangiwa.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Igunga, Godslove Kawiche baada ya kupokea taarifa kutoka kwa afisa elimu wa shule za sekondari Wilaya ya Igunga,Patricia Mbigili majina ya wanafunzi 747 kwamba pamoja na jitihada zake zote za kuwafuatilia wanafunzi hao lakini imeshindikana.

Aidha Kawiche amesisitiza pia kwamba haiwezekani idadi ya wanafunzi wote washindwe kuripoti shuleni wakati elimu inatolewa bila malipo kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne hivyo ni lazima wanafunzi wote wasakwe na kupelekwa shuleni.

Hata hivyo katibu tawala huyo amefafanua kuwa pamoja na jitihada zote ambazo amekuwa akizifanya mkuu wa Wilaya ya Igunga,John Mwaipopo za kuhamasisha wazazi kupeleka watoto wao shule, lakini baadhi ya wazazi wamekuwa wagumu kuzingatia maelekezo ya Serikali hivyo lazima hatua kali zichukuliwe dhidi yao.

Kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi kutoripoti kuanza masomo yao ya kidato cha kwanza,hivyo alilazimika kutoa muda wa siku saba kwa maafisa hao kuwasaka wanafunzi katika kipindi cha siku saba na kuwafikisha shuleni hata kama mwanafunzi atakuwa hana sare za shule atatumia nguo zake za nyumbani wakati mzazi wake akijipanga.

Alibainisha kwamba baada ya muda wa siku saba kumalizika kila afisa mtendaji wa kata atatakiwa kupeleka taarifa ofisi ya Mkuu wa wilaya na baadaye msako utaanza kwa wale watakaokuwa bado watoto wao hawajaripoti shuleni.

Naye Afisa Elimu shule za sekondari wilaya ya Igunga,Patricia Mbigili amesema jumla ya wanafunzi 5,310 walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza 2020/2021 ambapo kati ya hao wavulana walikuwa 2,365 na wasichana 2,945.

Kwa mujibu wa Mbigili hadi kufikia Machi,31,mwaka huu, jumla ya wanafunzi 4,563 wameripoti shuleni na kwamba kati yao, wavulana ni 2,036 na wasichana ni 2,527 na kuweka bayana kwamba jumla ya wanafunzi 747 wakiwemo wavulana 329 na wasichana 418 bado hawajaripoti kuanza masomo yao.

K