November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanawake wawezeshwa kuanza kilimo cha mboga mboga

Na Dotto Mwaibale,TimesMajira Online. Singida

WANAWAKE katika Kata za Sepuka na Irisya Wilaya ya Ikungi mkoani hapa, wameanza kuandaa shamba kwa ajili ya kilimo cha mboga mboga na matunda baada ya kuwezeshwa na Asasi ya Kilele inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA.

Wamefikia hatua hiyo baada ya kupatiwa mafunzo na asasi hiyo kwa kushirikiana na UN WOMEN pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, lengo likiwa ni kujikomboa kiuchumi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wakiandaa shamba hilo lililopo Kijiji cha Mnang’ana Kata ya Sepuka kwa ajili ya kilimo hicho, baadhi ya wanawake hao kutoka katika vikundi vya Mfuu, Mrumba, Wajifya na Misenga wametoa pongezi kwa asasi hiyo na halmashauri kwa kuwathamini kwa kuwapelekea mradi huo.

Katibu wa Kikundi cha Mrumba, Asia Gudo amesema mradi huo wameupokea kwa mikono miwili na kuwa wamefurahi kwani wanatarajia kunufaika kiuchumi na mazao watakayopata ambayo aliyataja kuwa ni nyanya, pilipili hoho na miche ya miembe watakapoyauza na fedha zitakazopatikana watawasomesha watoto wao, kununua mifugo na kujikimu kimaisha.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kikundi cha Mfuu, Mwahija Njiku amesema kupitia mradi huo waliowezeshwa na UN-WOMEN na TAHA, utawakomboa kiuchumi na kuwapunguzia mzigo wanaume katika majukumu ya kulea familia.

Naye Mayasa Omari, ambaye ni Katibu wa Kikundi cha Wajifya ameipongeza asasi hiyo kwa kuwapelekea mradi huo ambao ni endelevu na kuwa utawakomboa wanawake kwa namna moja ama nyingine.

Akizungumzia mradi huo Mtaalamu wa Kilimo wa TAHA Mkoa wa Singida, Mohamed Bakari amesema hivi sasa kwa kushirikiana na wanawake hao wapo katika hatua ya kufunga mifumo ya umwagiliaji katika mashamba manne na kuwa wamefikia hatua nzuri.

Ametaja mazao watakayoyapanda katika mashamba hayo kuwa ni nyanya maji, pilipili kichaa pamoja na vitunguu.

“Mazao haya yamekuwa zaidi ya moja kwenye eneo moja kwa sababu tutayatumia kama mashamba darasa, ambapo wakulima watakuja kujifunza ili nao wapeleke teknolojia hiyo maeneo mengine,” amesema.

Bakari amesema kwa kuwa kilimo hicho ni kipya katika wilaya hiyo, mwitikio wa wanawake hao ni mkubwa huku wakiwa na hamu ya kuona matokeo yake baada ya kupanda mazao hayo.