January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanawake watakiwa kuachana na mikopo ya kausha damu

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa Dar es Salaam Janeth Masaburi,amewataka Wanawake wa wilaya ya Temeke waache kukopa mikopo ya kausha damu badala yake wakope mikopo inayotambulika na Serikali ikiwemo taasisi za fedha.

Mbunge Janeth Masaburi, alisema hayo jimbo la Temeke wakati wa kuzungumza na Mama lishe wa Temeke stereo, alipofanya ziara sokoni hapo na kuwapa elimu ya kutumia nishati mbadala na majiko ya gesi.

“Nawaomba wanawake wenzangu mchukue mikopo inayotambulika na Serikali msichukue mikopo ya kausha damu mikopo hii wanawake inawaumiza riba yake kubwa”alisema Masaburi

Mbunge Masaburi alisema wanawake ni kiungo wa familia hivyo aliwataka washirikiane na kuwa wamoja na kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa Ilani ya chama cha Mapinduzi CCM.

Alisema katika ziara hiyo Mbunge Masaburi anatembea kuangalia miradi ya Serikali, changamoto na kugawa majiko ya gesi kwa mama lishe na Baba Lishe ili watumie nishati ya gesi waache kutumia mkaa.

Katika hatua nyingine Mbunge Masaburi amemtaka afisa Biashara Temeke kutimiza wajibu wake kwa kusimamia kanuni za afya katika soko la Temeke stereo huku akitaka tukemee na kuchukuia kauli mbiu ya Baba wa Taifa Ujinga ,Maradhi na umasikini ili tuweze kusonga mbele.

Akizungumzia Manispaa ya Temeke alisema inafanya vizuri sana kwa ushirikiano wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke ambapo, aliwataka watendaji kushirikiana na Wenyeviti wa Serikali za mitaa kutatua changamoto ngazi ya mtaa,kata kwa kushirikiana pamoja

Meneja wa masoko Manispaa ya Temeke Godfrey Aswikile alisema mikakati ya Manispaa ya Temeke mwaka wa Fedha 2023,2024 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Dkt.Samia Suluhu Hassan imeweka bajeti yake kwa ajili kuboresha miundombinu ya soko la Temeke stereo kuwa la kisasa na litachukua wafanyabishara wengi wa soko hilo .

Meneja Godfrey alisema soko la Temeke stereo lina wafanyabishara zaidi ya 5000 Manispaa ya Temeke kuna masoko 28 kati ya masoko 28 masoko 24 ya Serikali na masoko manne ya watu binafsi.