January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanawake Waaswa kuelimisha vijana kujiepusha na Rushwa ya Ngono

Na Mwandishi wetu, Timesmajira online

KATIKA kuelekea Siku ya wanawake Duniani, Wanawake Wameaswa kuelimisha vijana waliopo vyuoni na maeneo ya kazi kujiepusha na Rushwa ya Ngono kufanya hivyo kutasaidia kutokomeza kabisa tatizo hilo.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam jana na Katibu Msaidizi kutoka Tume ya utumishi wa Umma, Salvatory Kaiza wakati akifungua Mafunzo ya nidhamu na utaratibu wa undeshaji wa mashauri ya nidhamu sehemu za kazi yaliyoandaliwa na Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu (THTU)- wanawake Taifa kwa kushirikiana na Taasisi ya ustawi wa jamii.

Kaiza alisema ni jukumu la jamii hasa walezi na wazazi kukemea na kufichua vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto wa kike.

Aliongeza kuwa kesi za rushwa ya ngono zimekuwa zikitipotiwa mara kwa mara kutoka katika vyuo mbalimbali na mashauri yake yamekuwa yakifanyiwa kazi

“Nidhamu ni suala la muhimu sana kwa watumishi wa umma ili kufikia malengo ya taasisi, ni vyema wafanyakazi kuzingatia sheria, taratibu na kanuni mahali pa kazi ili kufanikisha utendaji wa kazi katika taasisi,kulinda utumishi wetu na tumalize utumishi wetu salama pia kuwalinda watoto wetu hasa wa kike waliopo vyuoni,” amesema Kaiza.

Kwa upande wake kaimu Mkuu wa taasisi ya Ustawi wa jamii Dkt Evantius Mgabuso amesema kuwa mafunzo hayo yametolewa ikiwa ni kuelekea siku ya wanawake ili kuweza kupunguza Mashauri yanayosababisha watumishi kuondolewa makazini.

“Mwanamke amekuwa mhanga mkuu pale mtumishi wa umma yeyote anapoadhibiwa akifanya makosa iwe yeye mwenyewe au iwe familia, hivyo ni jambo jema sana kwa mafunzo hayo kuandaliwa na wanawake wa THTU Taifa”amesema

Naye Kaimu Mratibu wa kamati ya wanawake Kutoka chama cha wafanyakazi wa Taasisi za elimu ya juu Tanzania (THTU) Roselyne Massam amesema, lengo la Mafunzo hayo ni kusaidia watumishi kuelewa umuhimu wa nidhamu mahali pa kazi, kupunguza migogoro kazini na ucheleweshwaji wa rufaa kwa mfanyakazi.

Massam aliiomba Tume ya Utumishi wa Umma kuongeza wafanyakazi wanaoshughulikia mashauri ya nidhamu sehemu za kazi ili kuongeza kasi ya utendaji na kupunguza ucheleweshwaji wa rufaa kwa mfanyakazi.

Katibu Msaidizi wa Tume ya Utumishi ya Umma, Salvatory Kaiza akizungumza na watumishi na watendaji wa Taasisi ya ustawi wa jamii