April 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanawake nchini wachangia asilimia 35 ya pato la taifa

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Wanawake nchini Tanzania wametajwa kuwa na mchango mkubwa katika Pato la Taifa ambapo takwimu zinaonesha kuwa asilimia 35 ya uchumi wa Tanzania unatokana na juhudi za wanawake ambao wanachangia asilimia 70 ya nguvu kazi ya kilimo ni wanawake hasa katika mazao ya chakula.

Mchango wa mwingine wa wanawake unajidhihirisha katika biashara, viwandani na katika huduma za kifedha kupitia utafiti uliofanywa na Chama cha Mabenki Tanzania (TBA) mwa ka 2022 umeonesha wanawake ni asilimia 47 ya wafanyakazi wote wa sekta ya fedha. Pia wanashika asilimia 10ya nafasi za kufanya maamuzi. Vile vile, wakiwa wajumbe katika bodi za wakurugenzi sawa na wastani wa wanawake wawili katika kila bodi.Hayo yamebainishwa leo Aprili 14, 2025 jijini Dodoma na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati aliposhiriki katika ufunguzi wa Mkutano wa mwaka wa Chama cha Wanawake katika Sekta ya Fedha (TAWiFA).

Pamoja na mafaniko hayo, Dkt. Biteko ametaja changamoto zinawakabili wanawake katika sekta ya fedha kuwa ni uhaba wa upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu, elimu duni ya masuala ya kifedha na uchache wa nafasi za kushiriki katika maamuzi ya Sera za Fedha.Amewanawake nchini kuzingatia misingi ya malezi kwa watoto wao kwa kuwapa nafasi sawa watoto wa kike na wa kiume ili kukabili changamoto zinazotokana na mila, desturi utamaduni.

“ Kwa kushirikiana na wadau wengine Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua za makusudi ili kutatua changamoto zinazomkabili mwanamke na hivyo kuchochea maendeleo” amesema Dkt. Biteko.

Amebainisha baadhi ya hatua hizo kuwa ni kuwaamini na kuwapa wanawake nafasi za juu za uongozi na maamuzi, kufanya Mapitio na Tathmini ya Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2000, kuandaa miongozo mbalimbali ikiwemo Mwongozo wa Ulinzi na Usalama wa Wanawake na Vijana Vyuoni uliozinduliwa mwaka 2023 na kutoa fursa nyingine mbalimbali za kifedha na kiuchumi kwa wanawake.Amesisitiza kuwa wanawake wanatakiwa kuwekeza zaidi katika mifumo ya kidigitali ili kuendana na mabadiliko ya kidigitali

“Naomba hapa nitoe rai kwenu kuwa, mkiwa mnaendelea kutekeleza majukumu yenu, msisahau kuhusu kuwekeza katika teknolojia. Maana Dunia ya sasa inazidi kwenda zaidi katika maisha ya kidigitali.

Hii itasaidia kurahisisha biashara na kufikisha huduma kwa wepesi hususan katika maeneo ya vijijini,”Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amesema kupitia mijadala na maazimio yatakayotolewa katika mkutano huo, zitapatikana mbinu mpya za kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya fedha na uchumi wa nchi kwa ujumla kupitia mabenki, kampuni za bima, masoko ya mitaji. Pamoja na mbinu na njia mbalimbali za fedha mtandao zinazotatua changamoto zinazomkabili mwanamke katika sekta ya fedha.

Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha, Hamad Chande amewapongeza wanawake nchini kwa kuanzisha Chama hicho kinacholenga kusaidia wanawake kiuchumi.Amewahakikishia kuwa Serikali imeandaa mazingira rafiki kwa wanawake katika ukuzaji wa uchumi “ Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa kutunga sera na sheria za kiuchumi ili wanawake na makundi mbalimbali yaweze kuimarika kupitia taasisi na vyama kama hivi.

Aidha, Serikali itaendelea kushirikiana nanyi ili kuimarisha TAWiFA ili kuhakikisha nafasi ya mwanamke inazidi kuwa juu katika jamii.”Rais wa Chama cha Wanawake katika Sekta ya Fedha (TAWiFA), Fikira Ntomola amesema kuwa wanawake nchini wameendelea kujishughulisha ili kuhakikisha sekta ya fedha nchini inakuwa.

Aidha, jamii inapaswa itambue uwekezaji kwa wanawake si hisani bali ni uwekezaji wa kimkakati kwa maendeleo ya Taifa.“ Tunaahidi kufikisha elimu ya fedha kwa wanawake katika maeneo mbalimbali nchini kwa kuandaa mafunzo na warsha kwa lengo la kuongeza uwezo wa kusimamia masuala yao ya fedha na biashara,” amesema Ntomola.

Ameongeza kuwa TAWiFA imedhamiria kuleta mabadiliko chanya kuhusu ushiriki wa wanawake katika sekta ya fedha, aidha wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka sera na sheria zinazochochea uchumi jumuishi na uwepo wa usawa wa kijinsia kiuchumi na kijamii.

“Tumekuwa tukiwajengea uwezo wanawake wa kuendesha biashara zao kiufanisi, kukuza biashara zao na kupanua wigo wao kuhusu sekta ya fedha,” amebainisha Ntomola.

Amewaomba wadau mbalimbali nchini kufungua milango ya fursa kwa wanawake, na kuwa TAWiFA ipo tayari kushirikiana nao kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha kwa umma, pamoja na tafiti za kuendeleza miradi ya kusaidia wanawake ili kujenga sekta ya fedha iliyo jumuishi.Makamu wa Rais wa Chama cha Wanawake katika Sekta ya Fedha (TAWIFA), Nangi Massawe amesema kuwa Chama hicho kinakutanisha wanawake katika sekta ya fedha ili kujenga sekta yenye usawa kwa manufaa ya Taifa.

TAWiFA kina jumla ya wanachama 204 na kimeendelea kuhakikisha wanawake wanashiriki katika sekta hiyo ili kuchochea maendeleo.