Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online, Shinyanga
BAADHI ya wajumbe wa Vyama Vikuu vya Ushirika vinavyojishughulisha na kilimo cha zao la Pamba nchini (TANCCOOP) wameonesha hofu kuhusiana na mstakabali wa vyama vya ushirika nchini baada ya Serikali kuruhusu mfumo huria kwenye uuzaji wa mazao ya wakulima.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kaimu Mrajis wa vyama vya Ushirika mkoani Shinyanga, Hilda Boniface ambayo ameitoa kwenye mkutano mkuu wa TANCCOOP kuanzia msimu wa mwaka huu wakulima hawatalazimishwa kupeleka mazao yao kuuza kwenye vyama vyao vya msingi (Amcos)
Wajumbe hao wamesema kufuatia uamuzi huo wa Serikali kuna uwezekano mkubwa wa Vyama vingi vya msingi vya Ushirika kuteteleka kutokana na kutoweza kuhimili ushindani kati yao na wanunuzi binafsi ambao hata hivyo mara nyingi humnyonya mkulima.
Pamoja na wajumbe kuridhia uamuzi huo wamedai Serikali imeutoa bila kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama kinachoiongoza serikali hiyo Chama cha Mapinduzi (CCM) ambayo moja ya ahadi zake kwa watanzania ni kuimarisha ushirika nchini.Mmoja wa wajumbe hao, Deogratias Didi kutoka Chama Kikuu cha Ushirika cha Chato na Biharamulo (CCU) mkoani Geita amesema uamuzi huo ni utaathiri kwa kiasi kikubwa mfumo wa ushirika hapa nchini na hautaendelea kuwa na maana tena.
“Maamuzi haya yana athari kubwa kwa ushirika hapa nchini, Ushirika ni Ilani ya uchaguzi ya CCM, kwa kweli naamini ushirika ukiboreshwa na ukasimamiwa vizuri ni mkombozi kwa mkulima na mtanzania kwa ujumla, nawaomba wakulima wetu waungalie ushirika kwa ukaribu,”
“Ushirika ni eneo pekee ambalo mkulima anaweza kupata faida kubwa pale anapouza mazao yake, na si kweli kwamba eti wana ushirika ni wezi, bali kuna watu wachache huchomeka watu wao wasiokuwa waaminifu ili wakaharibu sifa za ushirika, ninawaomba Rais Samia na Waziri Bashe waungalie ushirika, vinginevyo utakufa,” anaeleza Didi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taifa wa Shirikisho la Vyama vya ushirika nchini (TFC), Gishuli Charles amesema hatua ya kuruhusu wanunuzi binafsi kwenye zao pamba maarufu kwa jina la mabindo ina madhara kwa vyama vya ushirika pamoja na Serikali yenyewe.
Amesema mara nyingi wanunuzi binafsi wamekuwa na tabia ya kuwapunja wakulima kwa kutumia vipimo wanavyopimia mazao ya wakulima na hata pale vinapokaguliwa na wahusika hutumika kwa muda na wanapoondoka huviharibu vilevile ni vigumu kukusanya ushuru halisi kutoka kwao ikilinganishwa na unavyokusanywa kupitia Amcos.
“Ninashangaa kuona Serikali kuona inaruhusu tena wakulima kuuza mazao yao kupitia watu binafsi, sasa sielewi iwapo zile sababu za awali zilizokuwepo za kuwazuia kununua mazao moja kwa moja kupitia kwa wakulima kama zimeondoka, maana mwanzoni walikuwa wakinunua, ikabainika wanawapunja wakulima,”
“Kutokana na hali hiyo Serikali ikaagiza mazao yawe yanakusanywa kwenye vyama vya msingi vya ushirika ambako wanunuzi binafsi na makampuni makubwa watakwenda kununua kwa bei nzuri na kwa kutumia vipimo sahihi, hali hii pia iliwezesha kukusanywa kwa ushuru wa halmashauri kwa urahisi, kwa sasa sijui itakuwaje,” anaeleza Gishuli.
Kwa upande wao wenyeviti wa vyama vikuu vya ushirika mkoani Shinyanga (SHIRECU), Kwiyolecha Nkilijiwa na mkoa wa Singida (SIFACU) Yahaya Ramadhani wametoa wito kwa vyama vya ushirika kujiandaa ili kuweza kukabiliana na ushindani kati yao na watu binafsi.
“Kwenye ushirika kwa sasa hivi tunahitajika kujiimarisha, maana huko nyuma vyama vikuu vingi vilikuwa vimesinzia, awamu ya tano ilifufua vyama vingi, sasa tumeamka na tunatakiwa kuingia kwenye ushindani tunaomba basi angalao Serikali itengeneze mazingira rafiki ili tuweze kuhimili ushindani,” anaeleza Yahaya.
George Kihimbi Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Igembesambo, Bukene mkoani Tabora amesema vyama vingi vya ushirika bado ni vichanga, hivyo panahitajika nguvu ya ziada kuingia katika ushindani wa ununuzi wa mazao na watu binafsi.
Kihimbi amesema moja ya mfumo ambao iwapo ungeimarishwa ungeweza kuwakomboa wakulima hapa nchini, ni uuzaji wa mazao kwa mfumo wa Stakabadhi za ghala ambapo mkulima hupata bei nzuri na ungeimarisha vyama vya msingi vya ushirika.Kwiyolecha Nkilijiwa Mwenyekiti wa SHIRECU amesema kwa sasa hawana njia ya mkatao kutokana na uamuzi huo wa Serikali bali vyama vya msingi vya Ushirika vinapaswa kujipanga na kuhimili ushindani na kwamba iwapo watasimama vizuri wana uwezo mkubwa wa kuwashinda wanunuzi binafsi.
Awali katika mkutano huo, Kaimu Mrajis wa Ushirika Mkoani Shinyanga, Hilda Boniface aliwataka viongozi wa ushirika na vyama vya msingi (Amcos) kujiandaa kwa ushindani kwenye ununuzi wa zao la pamba katika msimu huu kwa vile mkulima hatolazimishwa tena kupeleka pamba yake kwenye chama cha msingi bali auze popote atakapoamua.
More Stories
Kambi ya wanasheria Katavi kuwajengea uwezo wananchi
Serikali yaimarisha uchumi wa kidigitali kukuza biashara mitandaoni
RAS Tanga aipongeza Lushoto DC kuvuka lengo mapato ya ndani