November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‘Wanasiasa acheni kutumia lugha yenye ukakasi’

Na Daud Magesa,TimesMajira Online. Mwanza

JUMUIYA ya Maridhiano Tanzania Mkoa wa Mwanza, kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 28 mwaka huu imewataka viongozi wa vyama vya siasa, waache kutumia maneno na lugha yenye ukakasi inayoashiria kuvunja amani.

Pia imeishauri Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kusimamia haki kwa weledi kwenye uchaguzi ili kuepusha amani isivurugike na kuonya vijana waache kutumika kisiasa kwa sababu, kila king’aacho si dhahabu badala yake wachague.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Alhaji Shekhe Mussa Kalwanyi wakati akitoa tamko la jumuiya kuelekea uchaguzi wa mwaka huu.

Amesema viongozi wa vyama vya siasa kipindi hiki cha kampeni, waepuke kutumia lugha na maneno yanayoweza kusababisha taharuki kwenye jamii na yanayoashiria kuvunja amani iliyopo nchini.

Alhaji Kalwanyi amesema, amani ni tunu muhimu inayopaswa kulindwa kwa namna na gharama yoyote, kwani bila amani hakuna mafanikio na maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

“Tarehe 28 Oktoba 2020 nawakumbusha Watanzania tukamchague kiongozi atakayethamini amani yetu na kuilinda kwa maslahi ya taifa letu na niwaombe viongozi wa dini, kuendelea kuiombea nchi yetu amani, kwani viongozi wa dini mnajua kuwa Mwenyezi Mungu ni kishikio na mwenye kumshika haanguki, hivyo tuendelee kuiombea nchi yetu,” amesema.