Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline Morogoro
WANASHERIA walioambatana na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ziara yake ya mkoani Morogoro wamekuwa msaada mkubwa kwa wananchi kwa kutoa elimu ya sheria na kuchukua changamoto zao kwa ajili ya kuzifanyia kazi.
Wanasheria hao wanaotoka kwenye Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Legal Aid walianza kuambatana na Rais Samia tangu kuanza kwa ziara yake kwa lengo la kusaidia wananchi wanaotoa kero za kisheria katika ziara hiyo.
Rais Samia amemaliza ziara yake mkoani Morogoro jana alitarajiwa. Akizungumza juzi akiwa kwenye mwendelezo wa ziara hiyo ya Rais, Beatrice Mpembo, ambaye ni Mkurugenzi wa Ufuatiliaji wa Haki wa Wizara ya Katiba na Sheria, alisema wamekuwa wakichukua kero mbalimbali za kisheria na kuzifanyia kazi.
Alisema timu hiyo ya msaada wa sheria katika ziara hiyo imekuwa ikitoa elimu ya masuala ya kisheria kwenye maeneo mbalimbali ambayo Rais anatembelea katika ziara hiyo ya siku tano.
“Timu yetu ya msaada wa sheria kwenye ziara hii ya mheshimiwa Rais inaainisha maeneo yanayohusu haki mbalimbali za kikatiba kwa lengo la kuishauri serikali ili kila mwananchi aweze kuzipata haki hizo kwa urahisi na kwa usawa,” alisema
Beatrice alisema Rais alipotembelea Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani humo timu hiyo ya Mama Samia Legal Aid imepata fursa ya kuainisha maeneo ya ushirikiano kati ya Wizara ya Sheria na Katina na chuo.
“Eneo mojawapo ni kuhamasisha wanafunzi wanaomaliza chuo hiki kujiunga na Chuo cha Sheria kwa Vitendo yaani Law School of Tanzania ambayo iko chini ya Wizara ya Katiba na Sheria ili kupanua wigo wa kupata wanasheria wa kutosha ambao wizara itawatumia kwenye kampeni hii,” alisema
Alisema mpaka kukamilika kwa ziara hiyo ya Rais wananchi wengi watakuwa wamenufaika na msaada wa kisheria ambao wamekuwa wakiutoa kila eneo ambalo Rais Samia ametembelea.
“Tumekutana na wananchi wengi sana na wamefurahi kupata elimu ya msaada wa sheria na wengine wametupa changamoto zao ambazo tumezichukua na kwenda kuzifanyia kazi na wananchi kwa ujumla wamefurahia sana ziara hii ya mheshimiwa Rais Samia,” alisema Beatrice.
Alisema kwenye ziara hiyo timu ya wanasheria hao imeambatana na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Pindi Chana.
Kampeni ya Mama Samia Legal Aid ni kampeni endelevu yenye lengo la kuwapatia wananchi elimu ya msaada wa sheria na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa wale ambao hawana uwezo wa kuweka mawakili kwenye mashauri yao.
Kaimu Mkrugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ester Msambazi, alisema hivi karibuni kuwa wananchi wanapopata elimu ya kisheria na ushauri, wanakuwa na uwezo wa kuelewa taratibu za kisheria na haki zao, hivyo kupunguza malalamiko na migogoro isiyokuwa na ulazima.
“Kampeni hii inalenga kusogeza huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi kwa njia rahisi na ya karibu. Kupitia kliniki za ushauri na elimu ya sheria, wananchi watapata fursa ya kushauriwa na wataalamu wa sheria bila malipo,” alisema
Alisema kampeni hiyo inalenga pia kujenga jamii yenye ufahamu zaidi na yenye uwezo wa kudai na kulinda haki zao za ardhi kwa mujibu wa sheria Kukuza usawa na haki katika jamii, kuheshimu matakwa ya marehemu, kuzuia migogoro ya mirathi, na kusimamia mali kwa njia inayofuata sheria na haki za kila mmoja.
“Wananchi wanahitaji msaada wa kisheria ili kupata haki zao kwa hiyo hii kampeni inatoa msaada wa kisheria kupitia vituo vya msaada, mawakili, na elimu ya kisheria, ikilenga migogoro ya ardhi, urithi, na haki za binadamu na inaongeza uelewa wa sheria na upatikanaji wa haki nchini Tanzania,” alisema.
****SIMULIZI YA WANUFAIKA WA SAMIA LEAGAL AID
“Nimefurahi sana kuwepo kwa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi napendekeza kama itampendeza Rais Samia hii isiwe tu kampeni maana kampeni inaisha muda ila ikiwa Taasisi ya kudumu itawasaidia sana wananchi wanyonge ambao wanapambana sana kusaka haki zao kisheria.”
Haya ni maneno ya Mkazi wa Kigamboni mkoani Dar es salaam, Lameck Kipiliango aliyefika kupata msaada wa kisheria katika Banda la Maonesho la Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia lililopo viwanja vya nanenane Nzuguni Jijini Dodoma.
Kipiliango anasema amefika katika banda hilo ili kusaidiwa kupata ufumbuzi wa mgogoro wake wa ardhi na Jiji la Dodoma.
“Nimefurahi nimepata msaada wa kisheria unaohusiana na mambo ya ardhi nimeona kama ni Mungu aliniongoza nije hapa nimefurahi sana, tunamshukuru sana mama ameleta kitu kipya huko nyuma hakikuwepo,”anasema.
Anasema wananchi wanapendekeza iwe taasisi ya kudumu na endelevu kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi kama ilivyo Taasisi ya Benjamin Mkapa.
Mwananchi Esther Lihofo anasema “Nimetembelea banda hili la sheria la Mama Samia nimekutana na Ofisa anaitwa Koku amenipa ushauri na elimu nzuri kuhusu masuala ya kisheria najipanga vizuri kwenye kuweka mirathi.”
Anasema mpango huo ni mzuri katika kuwasaidia wananchi wasio na uwezo ambao hawana uwezo wa kuweka Mawakili.
“Hapa kwa msaada wa mama tunapata msaada wa kisheria bure tunamshukuru Rais Samia kweli ni Rais wa wanyonge,”anasema.
Mkazi wa Area C Dodoma, Thomas, anasema katika maonesho ya nanenane amejifunza kupitia kampeni hiyo itasaidia wananchi wengi wasiokuwa na uelewa wa kisheria kuhusu masuala mbalimbali.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa kampeni hii ambayo imepiga kambi hapa nanenane Dodoma itawasaidia wananchi na watanzania kwa ujumla,”anasema.
Naye, Mkazi wa Hombolo, Lenard Hamis anasema amepata huduma nzuri kwenye banda la kampeni hiyo na amejifunza mambo ya kisheria ya kufuata na kutoa elimu kwa wananchi wenzao wa vijijini.
“Tumepewa namba za kupiga kwa ajili ya msaada wa kisheria tutawapa watendaji wasambaze kwa wananchi ili wanufaike na huduma hii ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, tunamshukuru sana Rais hakika mama anaupiga mwingi kwa wananchi wake,”anasema.
Mkazi wa Jiji la Dodoma, Yusuph Masatu, anasema amefarijika kupata huduma nzuri ambayo hakutegemea kuipa ya elimu ya masuala ya sheria.
“Nimshukuru Rais kwa kuona umuhimu wa kampeni hii, kweli watu ni wanyonge hawawezi kupata msaada wa kisheria kuwa na mawakili lakini ameliona hilo na kuleta kampeni hii ambayo itawasaidia sana watanzania tunashukuru sana,”anasema.
Mama Samia Legal Aid Campain ilianza kutekelezwa Aprili mwaka jana kwa kuanzia mkoani wa Dodoma na mpaka sasa tayari mikoa saba imefikiwa na mbali na Dodoma mikoa mingine iliyofikiwa ni, Manyara, Singida, Simiyu, Shinyanga na Njombe na Ruvuma.
Kampeni hiyo inachangia utawala bora ambao unajumuisha uwazi, uwajibikaji, na ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi na utekelezaji wa sheria na sera za umma.
Tangu ilipozinduliwa Aprili mwaka jana jijini Dodoma imeshawanufaisha wananchi zaidi ya 494,000 kutoka katika mikoa saba, wamepata suluhisho la migogoro huku migogoro ya ardhi ndio ikiongoza.
Kampeni hiyo imeshafikia mikoa saba, halmashauri 42, kata 452, na vijiji/mitaa 1,348 ambayo imewagusa wananchi kwa kuwapa msaada wa kisheria bure miongoni mwao wakiwemo wafungwa na mahabusu.
Takwimu za MSLAC zinaonyesha kuwa wafungwa 7,166 wanaume wakiwa 6,824 na wanawake 342 walifikiwa na kupewa msaada wa kisheria kwenye magereza mbalimbali nchini.
More Stories
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25