Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
WANASHERIA wanaoambatana na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ziara yake ya mkoani Morogoro wameendelea kuwa msaada kwa wananchi kwa kutoa elimu ya sheria na kuchukua changamoto zao kwaajili ya kuzifanyia kazi.
Wanasheria hao wanaotoka kwenye Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Legal Aid walianza kuambatana na Rais Samia tangu kuanza kwa ziara yake kwa lengo la kusaidia wananchi wanaotoa kero za kisheria katika ziara hiyo.
Rais Samia anaendelea na ziara yake mkoani Morogoro ambapo leo anatarajiwa kuongea na wananchi wa Ifakara na kesho anatarajiwa kuongea na wananchi wa Morogoro Mjini na anatarajiwa kuhitimiza ziara yake siku ya Jumatano.
Akizungumza leo akiwa kwenye mwendelezo wa ziara hiyo ya Rais, Beatrice Mpembo, ambaye ni Mkurugenzi wa Ufuatiliaji wa Haki wa Wizara ya Katiba na Sheria, alisema wamekuwa wakichukua kero mbalimbali za kisheria na kuzifanyia kazi.
Alisema timu hiyo ya msaada wa sheria katika ziara hiyo imekuwa ikitoa elimu ya masuala ya kisheria kwenye maeneo mbalimbali ambayo Rais anatembelea katika ziara hiyo ya siku tano.
“Timu yetu ya msaada wa sheria kwenye ziara hii ya mheshimiwa Rais inaainisha maeneo yanayohusu haki mbalimbali za kikatiba kwa lengo la kuishauri serikali ili kila mwananchi aweze kuzipata haki hizo kwa urahisi na kwa usawa,” alisema
Beatrice alisema Rais alipotembelea Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani humo timu hiyo ya Mama Samia Legal Aid imepata fursa ya kuainisha maeneo ya ushirikiano kati ya Wizara ya Sheria na Katina na chuo.
“Eneo mojawapo ni kuhamasisha wanafunzi wanaomaliza chuo hiki kujiunga na Chuo cha Sheria kwa Vitendo yaani Law School of Tanzania ambayo iko chini ya Wizara ya Katiba na Sheria ili kupanua wigo wa kupata wanasheria wa kutosha ambao wizara itawatumia kwenye kampeni hii,” alisema
Alisema mpaka kukamilika kwa ziara hiyo ya Rais wananchi wengi watakuwa wamenufaika na msaada wa kisheria ambao wamekuwa wakiutoa kila eneo ambalo Rais Samia ametembelea.
“Tumekutana na wananchi wengi sana na wamefurahi kupata elimu ya msaada wa sheria na wengine wametupa changamoto zao ambazo tumezichukua na kwenda kuzifanyia kazi na wananchi kwa ujumla wamefurahia sana ziara hii ya mheshimiwa Rais Samia,” alisema Beatrice.
Alisema kwenye ziara hiyo timu ya wanasheria hao imeambatana na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Pindi Chana.
Kampeni ya Mama Samia Legal Aid ni kampeni endelevu yenye lengo la kuwapatia wananchi elimu ya msaada wa sheria na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa wale ambao hawana uwezo wa kuweka mawakili kwenye mashauri yao.
More Stories
Waziri Mkuu: Tumieni matokeo ya tafiti za kisayansi katika utekelezaji wa mipango ya kitaifa
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu