Na Hadija Bagasha Tanga, TimesMajira Online
Mkuu wa wilaya ya Muheza Halima Bulembo amevionya vikundi vya watu wenye tabia ya kupita na kupotosha wananchi juu ya zoezi la upimaji na umilikishwaji wa ardhi linaloendelea katika kijiji cha muungano kilichopo kata ya Mlingano wilayani Muheza Mkoani Tanga.
Bulembo ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa akizungumza na wakazi wa kijiji hicho katika hafla ya kukabidhi hati 425 za umiliki wa ardhi kwa wanakijiji waliokamilisha hatua ya mwisho ya kulipia hati hizo zoezi ambalo limetekelezwa na Idara ya Ardhi na Kampuni ya Makazi Solutions.
Bulembo alisema umilikishwaji wa ardhi kisheria ni muhimu ili kuzuia migongano ya kimaslahi katika familia kwenye suala la umiliki wa ardhi hivyo wananchi wa wilaya ya Muheza wamesisitizwa kurasimisha makazi yao kisheria ili kuepuka migogoro ya ardhi inayojitokeza.
Bulembo amevikemea vikundi hivyo vya watu vinavyopita na kuwapotosha wananchi kijini hapo juu ya urasimishaji ardhi kwa maslahi yao binafsi jambo ambalo ni kunyume na mipango ya serikali juu ya umilikishwaji ardhi kwa wananchi.
“Nafahamu kuna vikundi vya baadhi ya watu vinawapotosha msiwasikilize wana maslahi yao binafsi mwanzoni tulisikiliza matatizo yao tukijua kwamba wana hoja katika kufuatilia kumbe wana maslahi yao binafsi na sisi wananchi bila kujua tunawasikiliza hivyo nyinyi leo mliopata hati mmelipia mmepata hati zenu hakuna mtu yeyote atakayekuja kuwasumbueni na kukuambia eti hili eneo ni la kwangu akitokea mtu wa namna hiyo njoo ofisini kwangu njoo na hati yako, “alisistiza DC Bulembo.
Alisema Suluhu ya kutatua migogoro ya ardhi itapatikana pale tu ambapo kila mwananchi atakuwa amerasimishiwa makazi yake na kupata hati yake kisheria.
Bulembo amewataka wananchi wa Muheza kuwa mabalozi wazuri wa wenzao kuhusu vikundi hivyo batili vinavyoipotosha jamii kuhusu urasimishaji wa ardhi.
Hata hivyo alieleza faida za wananchi kumiliki hati za ardhi kuwa ni pamoja na kuepuka migogoro ya ardhi na hivyo hakuna mtu yeyote atakayeingilia umiliki wa ardhi ya mtu ambayo imemilikishwa kisheria.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya Makazi Solutions Tanzania LTD Suleiman Said Pazzi alisema kampuni ya makazi solutions imeewa kazi hiyo ya upimaji na urasimishaji wa eneo hilo ambapo wamefanikiwa kuandaa michoro ipatayo 22 na viwanja elfu 25 na mashamba 1000 katika mradi wa shamba la urasimishaji makazi la Kilapula Azimio Geigliz lililokuwa shamba la mkonge ambalo lilifutwa na Rais wa awamu ya tano na kuelekeza wagawiwe wananchi.
Kwa mujibu wa Pazi mradi huo umefanikiwa kwa kuwa tayari wamerasimisha makazi yaliyokuwa holela na kupanga mji upya ikiwemo maeneo ya shule za msingi na sekondari, masoko, michezo, makaburi, na kuufanya mji huo kuwa wa kisasa.
“Kijiografia Kilapula ni mwanzoni mwa Tanga mjini hivyo Raskazoni sasa inakuwa hapa Kilapula kwahiyo tunatarajia kuwa na makazi mazuri sana hapa, “amebainisha Mkurugenzi Pazi.
Amebainisha baadhi ya Changamoto zinazokabili mradi huo mojawapo ikiwemo kupanda kwa thamani ya ardhi baada ya hatua hizo za upangaji mji ambapo kila mwananchi atahitaji kwa gharama anayoimudu jambo ambalo linakuwa changamoto kwa watu wenye kipato cha chini.
“Kabla ya mradi ekari moja ilikuwa ikiuzwa laki tano za kitanzania ila baada ya mradi mahesabu yetu ya ekari moja inayochukua Square mita 4050 ikipangwa zinatoka kama square mita 3000 kwa bei ambayo halmashauri inauza sasa hivi square mita moja ni shilingi 2000, kwa hiyo heka moja iliyokuwa inauzwa laki tano sasa vitatoka viwanja vyenye thamani ya kama milioni 6 hivi kwa ukubwa wa hilo eneo tafsiri yake ni nini ni kwamba ardhi imepanda thamani sana. “alisema Mkurugenzi huyo.
Baadhi ya watu waliokabidhiwa hati hizo akiwemo Noel Charles na Paul Lukindo walisema wana furaha kubwa kwa kuwa hivi sasa wana ardhi ambayo ni mali yao na urithi kwa watoto wao na ambayo haiwezi kuingiliwa na mtu yoyote.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Kijiji hicho Noel Bwilige alisema kuwa kuna kundi la wanakijiji wanaokubali zoezi hilo na ambao bado wana sintofahamu na wanahitaji kuelimishwa.
Bwilige aliimtaka Kamishna wa Ardhi kwenda katika kijiji hicho kufanya zoezi la kuwaelimisha wanakijiji waone kuwa ni halali na la serikali.
More Stories
CP.Wakulyamba ashuka Katavi na Nguzo nne za Uongozi
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Maandalizi ya mkutano mkuu CCM yapamba moto