Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na timu maalum ya kuzuia na kupambana na makosa ya mtandao limewakamata watuhumiwa 11 wa makosa ya kimtandao kufuatia ufuatiliaji mkali unaoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi na Timu hiyo Maalum
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Esalaam, Kamanda Kanda maalum ya polisi Dar es Salaam, ACP Jumanne Muliro amesema Watuhuhumiwa hao wamekuwa wakiweka taarifa zao za uzushi, uongo na upotoshaji kwenye luninga za mtandaoni zinazotambulika kwa majina ya BSUN Online TV, GATTU Online TV, TAMUTAMU online TV, KILIMANJARO online TV na nyinginezo.
“Mfano wa taarifa hizo ni kama “Rais Samia akosoa vikali utawala wa Rais JPM, aanika ukatili aliofanya (haukubaliki hata kidogo)” “IMEVUJA VIDEO, MBOWE APEWA SHAVU…!”, “DENI LA TAIFA LAIBUA MAZITO MWIGULU KUTUMBULIWA…!”, “GHAFLA MKE WA MAGUFULI AFA…!”, “ITAKUTOA MACHOZI UKWELI WOTE KIFO CHA MAGUFULI” Amesema ACP Muliro
Aidha Kamanda Muliro amesema Jeshi la Polisi na timu hiyo, limemkamata Alex Magoti (26) Mkazi wa Tabora Mjini na wenzake nane kwa tuhuma za kumiliki luninga za mtandaoni na akaunti za mitandao ya kijamii ambazo zimekuwa zikitumika kusambaza taarifa za uongo au uzushi kuhusu, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wakuu wa Serikali.
Mbali na hayo Kamanda Muliro amesema Jeshi la Polisi pia limemkamata LI NAIYONG (48) raia wa China, ambaye anatuhumiwa kujihusisha na shughuli za kuingilia mfumo wa mawasiliano kinyume na taratibu za nchi, na kuisababishia Serikali hasara ya kiasi cha Shilingi Milioni Mia mbili ishirini na moja laki moja sitini na tatu na mia sita (Tshs 221,163,600)
“Mtuhumiwa huyo amekuwa akituma vifaa visivyo rasmi kuwaunganisha watu kwa simu kufanya mawasiliano nje ya nchi kinyume na sheria za mamlaka ya mawasiliano Tanzania.”
Kamanda Muliro ameongeza kuwa Watuhumiwa hao wamekutwa wakiwa na vifaa mbalimbali ambavyo wanavitumia kufanya uhalifu huo, ikiwa ni pamoja na
Simu za mkononi 23, Laini za Simu 437 za makampuni mbalimbali ya huduma za simu zenye usajili wa watu tofauti tofauti, Kompyuta Mpakato 6, Sim Box 5, Routers 3 na Power Bank 1.
Pia Kamanda Muliro amesema Jeshi la Polisi limemkamata, Joseph Mzava (19) mkazi wa Kinondoni Dar es Salaam, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo cha Biachara Dar es Salaam (CBE), kwa tuhuma za kujinasabisha kuwa yeye ni Rais Mstaafu Jakaya Kikwete na kufanikiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kupitia mtandao kwa kutumia laini za simu zenye usajili usio na majina yake.
Jeshi la Polisi limeendelea kutoa rai kwa Wananchi kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii, pamoja na kuzingatia maadili ya taaluma ya habari na sheria zinazohusika kuepuka kuchapisha taarifa za uongo na zile zitakazo zua taharuki kwa umma ambapo Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali kwa mtu/watu wote watakao vunja sheria, kanuni na miongozo inayoelekeza matumizi sahihi ya mitandao.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa