December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanaohifadhi, kuajiri wahamiaji aramu waonywa

Na Suleiman Abeid, TimesMajira, Shinyanga

IDARA ya Uhamiaji Mkoani Shinyanga imekemea tabia ya baadhi ya watu wanaowaajiri kinyume cha sheria wahamiaji haramu kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo uchungaji wa mifugo hivyo yeyote atakayekamatwa sheria kali zitachukuliwa dhidi yake.

Onyo hilo limetokana na Idara hiyo wiki iliyopita kukamata wahamiaji haramu wapatao 24 ambao baadhi yao walikutwa wameajiriwa maeneo ya vijijini kufanya shughuli za kilimo na wengine kwenye uchungaji wa mifugo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Uhamiaji mkoani Shinyanga, Rashidi Magetta imesema, ukamatwa kwa wahamiaji haramu hao kunatokana na msako maalumu uliofanyika mkoani Shinyanga ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa walifikishwa mahakamani na kati yao tisa walihukumiwa kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka miwili gerezani na wengine 15 walirejeshwa nchini kwao Burundi baada ya kubainika walikuwa na umri chini ya miaka 18.

“Idara ya Uhamiaji Shinyanga, tunawaonya wananchi wajiepushe na tabia ya kupokea na kuwahifadhi wahamiaji haramu wanaoingia hapa nchini kinyume cha sheria, maana kwa ye yote atakayebainika aelewe mkondo wa sheria utafuatwa na wanaweza kupata adhabu kubwa,”.

“Ni vyema wananchi wakaelewa kuwa wahamiaji haramu daima wapo kwa maslahi yao na ya watu waliowaleta hapa nchini, maana wanaweza kufanya lolote baya bila kuweka maanani maslahi ya nchi yetu, na ikizingatiwa kuwa katika kipindi hiki ni cha uchaguzi hapa nchini wanaweza kusababisha kuvuruga uchaguzi kwa matakwa ya matajiri wao,” ameeleza Magetta.

Amesema, katika msako uliofanyika katika wilaya za Kahama na Shinyanga baadhi ya wahamiaji waliokamatwa walikuwa tayari wameiingia vijijini mbali na makao makuu ya Wilaya za Kahama na Shinyanga ambako walikuwa wamehifadhiwa na wenyeji.

Pia walibaini baadhi ya wahamiaji haramu hao walikuwa ni watoto ambao walikuwa wameajiriwa kufanya kazi za kilimo, shughuli za uchungaji wa ng’ombe na wengine kufanya biashara ndogo ndogo za uchuuzi kwenye maeneo ya migodi, magulio na gereji.

Pia amewaomba raia wema wenye mapenzi na nchi yao wasisite kutoa taarifa wakati wowote pale watakapowaona wahamiaji haramu wakiwa wamehifadhiwa au kuajiriwa kazi mbalimbali kinyume cha sheria ili hatua za kuwakamata ziweze kuchukuliwa mara moja.