January 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanaofariki kwa kunywa sumu waongezeka Kilimanjaro

Na Allan Vicent,TimesMajira Online,Siha

WANANCHI Wilayani Siha mkoani Kilimanjaro wamesikitishwa na ongezeko la vitendo vya watu kunywa sumu na kukatisha maisha yao huku rika la vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa likiongoza.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi wa wilaya hiyo wamedai kuwa matukio ya watu kunywa sumu yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku katika maeneo mbalimbali wilayani humo huku kundi la vijana likiwa ndio waathirika wakubwa.

Wamesema kuwa Novemba 10 mwaka huu, Thadeus Mushi (33), mkazi wa Merali Sanya Juu wilayani humo alikunywa sumu aina ya Gramoson na kufariki huku ikidaiwa chanzo ni ugomvi wa kifamilia

Salome Shayo na Juma Hussein wakazi wa Sanya Juu wameeleza kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikileta hofu na kuacha simanzi kubwa miongoni mwa jamii.

‘Haipiti wiki utasikia fulani kafa kwa kunywa sumu au kalazwa, tunaomba viongozi wa dini watusaidie kukemea tabia hiyo na wafanye maombi au dua maalumu katika nyumba za ibada ili kuiponya jamii, na washauri wale wenye changamoto za kimaisha wasikatishe uhai wao, bali waeleze wazi tatizo ili wapewe ushauri’, amesema Hussein.

Ofisa Ustawi wa Jamii Wilayani humo, Peter Msaka amewataka wakazi wa wilaya hiyo kuacha kuchukua maamuzi ya kujiua bali wale wenye matatizo wawaone wataalamu ili wawasaidie kutatua changamoto zao ikiwemo kupewa ushauri wa kitaalamu.

Amewataja baadhi ya sababu zinazoelezwa kuchangia vijana kunywa sumu kuwa ni ugomvi wa kifamilia, wivu wa kimapenzi na msongo wa mawazo hivyo akatoa wito kwa wale wenye changamoto za kimaisha kufika ofisini kwake ili wapewe ushauri wa kisaikolojia.

Mganga Mfawidhi wa hospital ya wilaya hiyo, Dkt. Nsubili Mwakapeje amesema vifo vitokanavyo na kunywa sumu vinaweza kuepukika kwa kujiua sio suluhu ya changamoto ya mtu.

Amesisitiza kuwa vijana wenye msongo wa mawazo au matatizo mbalimbali wamekuwa wakipewa ushauri nasaha na kutofikia hatua hiyo.

‘Tunaangalia uwezekanao ili watu wanaokunywa sumu na kupona wachukuliwe hatua,”amesema.

Amefafanua kuwa kuanzia Januari hadi Novemba 12 mwaka huu watu waliokunywa sumu za aina mbali mbali ikiwamo Gramoson walikuwa 59 ambapo wanaume walikuwa 29 na wanawake 30 kati ya hao 17 waliofariki dunia.