October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanaochimba visima wapeleke sampuli TAEC kupima viashiria vya mionzi

Na Joyce Kasiki,Dar es Salaam

AFISA Tafiti wa Tume ya Nguvu za Atomu nchini (TAEC) Dkt.Lazaro Meza  imewataka wananchi wanaochimba visima,kupeleka sampuli za maji ya visima hivyo kabla ya kuyatumia ilo zipimwe kujua kama yapo salama au yana viasili vya mionzi.

Dkt. Meza amesema iwapo kuna mionzi kwenye maji hayo inaweza kusababisha   magonjwa ya saratani na mengine mengi.

“Kama maji yamechimbwa   katika eneo lenye viasili vya mionzi muhusika alete sampuli yake TAEC tuone kama yapo salama ili kuwakinga watumiaji dhidi ya maradhi wanayoweza kuyapata.”amesema Dkt.Meza

Aidha amesema Tume hiyo inatumia maonesho hayo kutoa elimu kwa umma ili kuwapa  uelewa kwa wananchi kuhusu matumizi salama ya teknolojia ya mionzi na madhara yanayoweza kupatikana.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TAEC, Peter Ngamilo amesema,TAEC wanaendesha zoezi la kupima maji ya visima nchi nzima ili kuona kama yana viasili hivyo vya mionzi.

Aidha amesema, zoezi hilo linatekelezwa kupitia Sheria ya Nguvu za Atomu namba 7 ya mwaka 2003.

“Chini ya ardhi kuna vitu vingi,kuna  madini ya Uranium, hivyo maji yanaweza kuchimbwa na kukutana na madini ya mionzi lakini asijue.”amesema Ngamilo

Amewaasa wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalam wanaopita kufanya kazi hiyo ya kupima maji ili kurahisisha na kufanikisha zoezi hilo.

Kwa mujibu wa Ngamilo TAEC wamekuwa wakitoa vibali vya uingizaji, usafirishaji, umiliki wa vyanzo vya mionzi nchini, kufanya kaguzi mbalimbali katika maeneo yanayotumia vyanzo vya mionzi na kupima viasili vya mionzi kwenye mnyororo wa bidhaa ili kulinda wananchi dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi.

Vile vile amesema  pia wanafanya kazi ya kupima viwango vya mionzi kwenye minara ya simu na rada za mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wanaokaa karibu waendelee kubaki salama dhidi ya madhara ambayo yanaweza kusababishwa na mionzi.

Ngamilo amesema taasisi hiyo pia inawalinda wafanyakazi ambao wanafanya kazi kwa kutumia vyanzo vya mionzi katika shughuli zao za kila siku ikiwemo kwenye vituo vya afya, migodi, bandari, viwanja vya ndege .