Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
RAI imetolewa kwa wananchi Mkoani Mbeya kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara kwa kuwa wengi hufikiri wana afya njema wawapo majumbani jambo ambalo sio kweli.
Imeleezwa kuwa wengi wao baada ya vipimo walipofika kwenye huduma hii wamekutwa na changamoto mbambali za kiafya.
Akiongea leo,Novemba 15,2023 wakati wa maadhimisho ya siku ya kisukari Duniani Mratibu wa zoezi hilo ,Dkt.Alumbwage Nyagawa amesema lengo kubwa ni kusogeza huduma kwa wananchi ili waweze kupima afya zao .
“Kwasababu watu wengi wanakaa majumbani wanajiona wapo sawa lakini kwa uhalisia wanakuwa na changamoto za kiafya,”Dkt. Nyagawa
Amesema lengo kubwa ni kusogeza huduma kwa wananchi na kuhakikisha wananchi wanapata nafasi ya kupima afya zao pamoja na kupatiwa elimu, uchangiaji damu sambamba na huduma za upimaji wa magonjwa mbalimbalimbali yasiyo ambukiza.
“sisi kama hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya tumekuja kusogeza huduma kwa wananchi ili kuwawezesha kupima afya, kutoa elimu, pamoja na wao kuweza kuchangia damu,”amesema Nyagawa.
Epafra Isaya ni mwananchi mwenye uziwi aliyejitokeza kapata huduma ya upimaji wa afya amesema amefurahishwa na huduma nzuri alizopata mahali hapo kwa kuwa amepata nafasi ya kupima shinikizo la damu, ugonjwa wa kisukari, hivyo amefurahishwa na huduma hizo kwa kuwa wao viziwi wamekuwa wakipata wakati mgumu sana kupata elimu juu ya magonjwa yasiyoambukiza.
“Mimi nimefurahi kwasababu sisi viziwi mara nyingi hatuna uelewa wa magonjwa haya yasiyoambukiza hivyo tunashukuru hospitali ya kanda kwa huduma hii,”amesema.
Nae Jeofrey Simime ameishukuru Serikali ya Awamu ya 6 chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kusema jambo hili linatija kwa jamii kwa kuwa mtu unaweza ukawa unaishi ukidhani uko salama lakini kumbe una changamoto za kiafya.
“Naishukuru Serikali yetu ya Awamu ya sita kwa kutuletea huduma hii ya vipimo kwa wananchi ili kufanya uchunguzi wa afya zao kwa kuwa jambo hili linatija kwa jamii, mtu unaweza ukawa unaishi ukidhani uko salama kumbe unamagonjwa,” amesema Simime
Tarehe 14 Novemba kila mwaka, duniani kote huadhimishwa Siku ya Kisukari Duniani,Maadhimisho haya yanafanyika kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu kisukari, kuhamasisha watu kuchukua hatua za kuzuia na kudhibiti ugonjwa huo, na kushirikiana katika kupambana na changamoto zinazowakabili watu wanaoishi na kisukari.
Katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, maadhimisho ya Siku ya Kisukari Duniani yalikuwa ya kipekee na yenye tija ambapo hospitali kupitia timu ya wataalamu wa afya imetoa elimu na ushauri kuhusu kisukari, chunguzi wa afya bila malipo pamoja na uchangiaji damu salama kwa jamii.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba