January 2, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi watakiwa kuimarisha ulinzi na usalama

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amewataka wananchi wa Wilaya ya Ileje kushirikiana kuhakikisha wanaimarisha ulinzi na usalama kila siku katika maeneo yao.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa maelekezo hayo leo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Ileje Mkoani Songwe akiwa katika ziara yake mkoani humo.

“Ni jukumu letu kila mmoja tujipange vizuri kuhakikisha kwamba nchi zetu 2 zinabaki kuwa salama”

Aidha Waziri Majaliwa amesema kutokana na Wilaya ya Ileje kupakana na nchi jirani ya Malawi, amewataka wananchi hao kuendelea kuimarisha mahusiano ili biashara ziweze kufanyika kwa urahisi.

Amesema Wilaya ya Ireje na Nchi ya Malawi mahusiano yao yameendelea kuimarika hasa ushirikiano ulipo kati ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Chikwale kwa kuendelea kufanya mazungumzo ambayo yatapelekea kufungua milango ya Biashara nchini Tanzania.

“Nchi yetu Iko salama, na ninapokuwa hapa Ileje, najua Ileje ni Wilaya inayopakana na nchi jirani hata hivyo mpaka wetu upo salama, mahusiano yetu ya Tanzania na Malawi yameendelea kuimarika na viongozi wetu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Chikwale wana mazungumzo mazuri na mshikamano huu ukiendelea hapa Ileje patabadilika kwa Kasi kabisa kwasababu tutafungua milango ya mataifa ya nje kuingia Tanzania na kufika hapa Ileje” amesema Waziri Mkuu Majaliwa

Mbali na hayo, Waziri Mkuu Majaliwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kusimamia ujenzi wa jengo la Halmashauri lililokwama kujengwa kwa mwaka mzima kwani wananachi wanahitaji kuona mabadiliko ya majengo mapya.

Kadhalika Waziri Majaliwa amesema Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amenunua magari ya wagonjwa ambapo Wilaya ya Ileje itapata magari mawili Moja la kubebea wagonjwa kwa kuwafata wagonjwa vijiji kuwaleta Wilayani na lingine kwaajili ya Mkuu wa Afya kwaajili ya ufuatiliaji utendaji wa vituo vya Afya na zahanati.

Pia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemtaka Afisa wa LATRA Wilaya ya Ileje kuja na mpango rasmi kuhusu nauli za mabasi kupanda katika Wilaya hiyo.

Waziri Majaliwa amesema wananchi hao wamekua wakilalamika nauli kupanda kutoka 2500 hadi 3000.