January 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi washauriwa kuandika miradhi

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

WANANCHI wametakiwa kujenga utamaduni wa kuandika wosia na kuachana na dhana potofu kwamba kuandika wosia ni unajitabiria kifo.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Kujitegemea wa Tanganyika(TLS) Mwanza Chapter, Wakili Lenin Njau kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa Kisheria yanayofanyika Jijini Mwanza kuanzia Novemba 12 hadi 18 mwaka huu yakiwa na kauli mbiu isemayo ‘Usimamizi bora wa mirathi kwa maendeleo ya familia’ ambayo imebeba ujumbe unaogusa maisha ya jamii ya kila siku.

Wakili Njau amesema, mara nyingi tatizo la mirathi huwa kubwa endapo marehemu hajaacha wosia wa aina yoyote ambapo faida ya kuandika wosia ni pamoja na wewe mwenyewe kuamua kwa hiari yako mali zako ziende kwa nani badala ya kuacha jukumu hilo kwa msimamizi wa mirathi ambaye anaweza kugawa kinyume na matakwa yako na hivyo kupelekea dhuluma kwa familia yako au warithi wako halali uliowaacha hapa duniani.

“Napenda kutoa wito kwa wananchi wote na watu wote wakike na wakiume maana imejengeka dhana potofu kwamba mara nyingi wanaume ndio hufa kwanza kabla ya wake zao na hivyo wanawake wengi kuwahimiza wanaume zao waandike wosia na wao kujisahau,hivyo tuachane na dhana potofu kwamba kwa kuandika wosia wako basi eti unajitabiria kifo,hii haina ukweli wa aina yoyote kwa sababu kifo kipo tu hakuna mantiki yoyote endapo tutatumia nguvu kubwa kwa kufanya kazi kwa bidii na kutafuta mali halafu yushindwe kuacha wosia wa namna gani ungependa mali hizo zigawanywe pindi unapofariki,” amesema Wakili Njau.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella, amesema suala la mirathi linamgusa kila mmoja na ndio sababu wanazungumzia umuhimu wake katika maadhimisho hayo kwa mwaka huu huku wanawake wamekuwa wahanga wakubwa linapofika katika hali ya kufuatilia mirathi hasa baada ya kuondokewa na wenzi wao.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella akizungumza kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria yanayofanyika Jijini Mwanza kuanzi Novemba 12 hadi 18 mwaka huu . (Picha na Judith Ferdinand).

Mongella amewataka wananchi kuendelea kujenga tabia ya kufuatilia na kupata elimu ya msaada wa kisheria,kuendelea kuwatumia wadau mbalimbali ambao wanatoa msaada huo katika jamii huku serikali inaunga mkono jitihada mbalimbali zinazoendelea kuhakikisha wananchi wanapata elimu na ufahamu juu ya suala hili ambapo asasi za kirai ziwafuate wananchi walipo ili kuwa hudumia.

“Suala la mirathi limekua na changamoto nyingi sana zinazosababisha migogoro ambayo hupelekea wakati mwingine kuvunja mahusiano ya kindugu,kijamii na hata kusababisha vifo hali inayopelejea kuathiri mifumo mbalimbali ya maisha kijamii,kiuchumi,kiutamadunj na kisaikolojia, serikali yetu kwa kushirikiana na asasi za kirak itaweka mazingira muafa katika kutoa elimu ya msaada wa kisheria kwa wananchi ili kuleta usimamizi bora wa mirathi kwa maendeleo ya familia,” amesema Mongella.

Pia amesema katika utoaji wa msaada wa kisheria Shirika la Kivulini kuanzia 2016 hadi Julai 2020 kwa upande wa kesi za mirathi lilipokea kesi zipatazo 128 kutoka kwa wanaume na 171 kwa wanawake ambapo kati ya hizo kesi 66 za wanaume na 84 za wanawake zilizofunguliwa zilishughulikiwa hatahivyo kesi 59 za wanaume na 62 za wanawake zilipewa rufaa kwenda sehemu mbalimbali na kesi 13 za wanaume na 25 za wanawake zinaendelea.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za wanawake na wasichana la Kivulini, Yassin Alli amesema, kumekuwa na changamoto ya mjane ama mtoto wa marehemu ambaye alikuwa ameajiriwa sehemu fulani kuombwa barua kuthibitishwa kazini,banki statemate( taarifa za kibenki) ambayo yeye sio mhusika pamoja na hati ya malipo ya mshahara ya miezi mitatu na kitambulisho cha nida hali inayokwamisha masuala mazima ya mirathi hivyo aliomba kuondokewa kwa vikwazo hivyo.

“Kitambulisho halali ninachojua mtu anapokuwa ameisha kufa(amefariki) ni cheti cha kifo halafu bado unaombwa kitambulisho,mfano tuna kesi moja ambayo aliombwa barua ya kuthibitishwa kazini ya mwaka1976 na vitu vingine,na eneo jigine linalonisikitisha ni kuwa baada ya kuwa tumempa msaada wa kisheria na akawa ameshinda,”.

Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za wanawake na wasichana la Kivulini Yassin Alli

“Changamoto ikaja kuwa pesa ambazo zinapaswa kutoka kwenye mfuko wa hifadhi wa jamii na benki zikawekwa kwenye akaunti ya mahakama tena akaambiwa kuwa anatakiwa vyeti(certification),hukumu si ingetumika kama certification niwaombe mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa,waajiri wa sekta binafsi na serikali wanauwezo wa kufikiwa na mahakama kwa kutaka nyaraka hizo za mtumishi wao ambaye ni marehemu nazani ni matakwa halali ya kisheria badala ya kusema mtoto au mama aliyefiwa kiukweli hilo ndio ombi letu,” amesema Yassin.