Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline Mara
UVUVI wa samaki wa Vizimba unaohamasishwa na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Mkoani Mara Prof. Sospter Muhongo umetajwa na Wananchi wa Jimbo hilo kuwa, ni njia bora ya kukuza uchumi jimboni humo na kuwaletea Wananchi maendeleo.
Pia uvuvi huo umebainishwa kuwa njia bora ya kusaidia kuondokana na tatizo la ajira ikiwemo kwa vijana na kuwaletea maendeleo ya kiuchumi iwapo watajikita na uvuvi huo kikamilifu. Kutokana na uwepo wa Ziwa Victoria ndani ya Jimbo hilo ambalo ni fursa nzuri ya kuleta mageuzi chanya ya kiuchumi kupitia uvuvi na kilimo cha umwagiliaji.
Wameyasema hayo Februari 20, 2025, wakati wakizungumza na MajiraOnline kueleza shauku yao kuhusu uvuvi wa samaki wa Vizimba ambao umeendelea Kuhamasishwa na Prof. Muhongo kutokana na kupungua kwa samaki ndani ya ziwa Victoria.
Juma Masaba ni Mkazi wa Kijiji cha Busekera kata ya Bukumi amesema kuwa, anaunga mkono dhamira ya Mbunge wa Jimbo hilo Prof. Sospter Muhongo ambaye amedhamiria kuona kata 18 Kati ya 21 ambazo zinafursa nzuri ya kutumia rasilimali ya Maji ya Ziwa Victoria kufanya uvuvi wa Samaki kwa Vizimba ili uwanufaishe Wavuvi na wananchi jimboni humo.
“Niwazungumzie pia vijana ambao Wana Changamoto ya ajira hasa wanaomaliza vyuo vya Kati na vyuo vikuu. Badala ya kulalamika namna gani wapate ajira, ni vyema wakajiunga vikundi wakatafuta fursa ya mikopo na kujiajiri katika uvuvi huu, badala ya kusaka ajira ambazo kwa sasa upatikanaji wake si mwepesi.”amesema Masaba.
Jesca Fabiani Mkazi wa Kata ya Etaro amesema, uvuvi wa samaki wa Vizimba unafaida pia katika suala zima la uhifadhi wa mazingira kwani uvuvi huo unasaidi kuhifadhi mazingira ya maji kwa kuzuia Uvuvi wa kupindukia. Ambapo, samaki wanakuwa katika maeneo yaliyolindwa na kuweka uendelevu wa rasilimali zilizoko majini kwa faida ya baadaye.
“Niwaombe wavuvi wakiwemo vijana,waingie kwenye uvuvi wa Vizimba,wote hawawezi kupata ajira serikalini au katika makampuni. Na pia Wavuvi wanaofanya uvuvi wasiufanye kwa mazoea, Vizimba hutoa nafasi ya kuzalisha samaki kwa wingi na kufanya Wavuvi wapate samaki wengi wenye ubora ambao watawauza kwa tija na kukuza kipato chao.”amesema Mwita Erasto Mkazi wa Nyegina Musoma Vijijini.
“Tunaye Mbunge ambaye ni mpenda maendeleo, hapendi kuona wavuvi na Wananchi wanavua samaki kwa mazoea. Shabaha yake ni kuona Wananchi wanapata maendeleo kutokana na uvuvi wa Kisasa. Hili pia serikali imeliunga mkono kwa dhati kabisa ili kwamba sekta ya Uvuvi iwe na mchango chanya wa maendeleo si tu kwa Wavuvi, bali pia katika uchumi wa Nchi.” amesema Joachim Sadick Mkazi wa Kijiji cha Muhoji.
Ashura Mafuru Mkazi wa Busambara amewaomba Wananchi wa Musoma na Mkoa wa Mara wanaojihusisha na uvuvi, kuachana na tabia ya uvuvi haramu na kushiriki kikamilifu kupiga vita uvuvi huo ili kulinda rasilimali zilizoko ndani ya ziwa Victoria kwa manufaa endelevu.
Februari 17, 2025 Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Muhongo kupitia taarifa yake ailiyoitoa kwa Wananchi alisema kuwa,kutokana na kupungua kwa samaki ndani ya Ziwa Victoria Jimbo hilo limeweka malengo ya kuanzisha na kuendeleza uvuvi wa Vizimba katika kata 18 Kati ya 21 ambazo zina fursa nzuri ya kutumia rasilimali ya Maji ya Ziwa hilo kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi kwa Wananchi na Taifa pia.
“Upungufu wa samaki haupo tu ndani ya Ziwa Victoria, bali ni tatizo kubwa ulimwenguni kote! Bahari, maziwa na mito ya Duniani kote ina upungufu mkubwa wa samaki. Kwa hiyo sasa takribani nusu (ca. 50 ) ya samaki duniani kote wanapatikana kupitia ufugaji wa samaki ndani ya bahari, maziwa nakadhalika (Acquireculture fish farming)”amesema Prof. Muhongo.
“Kata 18 kati ya Kata 21 za Jimbo letu zina ufukwe wa Ziwa Victoria. Kwa hiyo, asilimia 85.7 (85.7%) za Kata zetu zina fursa nzuri za kutumia raslimali za maji ya Ziwa hili. Malengo yetu
ni kwamba Kata 18 kati ya 21 za Jimboni mwetu kuanzisha na kuendeleza Uvuvi wa Vizimba ndani ya Ziwa Victoria.”amesema Prof.muhongo.
Alisema Mitaji ya Uvuvi wa Vizimba kupatikana kutoka kwa Mitaji ya watu binafsi ambapo vizimba 10 vimeishaanza uzalishaji. Pia kutoka mikopo nafuu ya Serikali Kuu na vizimba 8 tayari vimetayarishwa na kuwekwa Ziwani. Na Uzalishaji utaanza ndani ya miezi 3 ijayo. Mitaji kutoka mikopo mizuri ya Benki za Biashara CRDB & NMB Mikopo 10 ya vizimba 50 itatolewa hivi karibuni.
Pia Prof.Muhongo pia alibainisha baadhi ya wavuvi wa vizimba wa Musoma Vijijini wamemueleza Mbunge huyo kuwa, kwenye kizimba kimoja chenye kipenyo cha mita 10 (10m-diameter) wamefanikiwa kuvuna tani 12 za samaki wenye thamani ya Shilingi za Kitanzania Mil.100.
More Stories
Mpango mahsusi wa Taifa kuhusu Nishati wajadiliwa
Mwenyekiti CCM, Mbunge Rorya wavuruga mafunzo ya makatibu
Serikali ,Washirika wa Maendeleo waweka mkakati utekelezaji Dira ya 2050