Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Mbeya
MKUU wa Tawi la Utawala Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Brigedia Jenerali Hassan Mabena ameipongeza serikali kwa kuondoa kiingilio katika maonyesho ya wakulima maarufu kama Nane Nane huku akiwaasa wananchi kujitokeza kwa wingi kufika kwenye maonyesho hayo hasa katika Banda la JKT ambako watapata maarifa katika maeneo ya Kilimo,mifugo na uvuvi.
Brigedia Jenerali Mabena ambaye amemwakilisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Mkuu wa JKT amesema hatua hiyo itaongeza ari kwa wakulima na wananchi kwa ujumla kufika katika maonyesho hayo ambayo Kitaifa yanafanyika mkoani Mbeya katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya na kujifunza masuala mbalimbali ya kilimo,ufugaji na uvuvi na hivyo kuleta tija kwenye maeneo hayo.
“Imeshatangazwa kwamba hakuna kiingilio kwenye maonyesho haya,nawasihi wananchi hususan wakulia wajitokeze kwa wingi kwenye maonyesho hasa kwenye banda letu la JKT ,watapata maelezo ya kina kutoka kwa wataalam wetu kuhusu masuala ya kilimo,ufugaji na uvuvi ili nao wakaongeze tija kwenye shughuli zao.”amesema Birigedia Jenerali Mabena
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango kuzindua sherehe za maonyesho hayo,Brigedia Jenerali Mabena amesema,maonyesho hayo yanatoa fursa kwa wananchi kuona pembejeo na zana za kilimo mifugo na uvuvi kwa jili ya kujifunza mbinu bora za uzalishaji wenye tija kwa mazao ya kilimo,mifugo na uvuvi.
Aidha ameipongeza Serikali chini ya uongozi wa Amiri Jeshi Mkuu Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kipaumbele katika sekta hizo kwa kuongeza bajeti kila mwaka ili kuleta tija.
“Sisi sote ni mashahidi ,2022/23 serikali ilitenga bajeti kubwa katika maeneo hayo na hata katika mwaka huu wa fedha imeongeza fedha ambazo zinakwenda kuleta uhakika wa usalama wa chakula nchini na hivyo kuleta utoshelevu wa chakula na ziada kuuzwa nje na kuleta fedha za kigeni ambazo zitatumika katika maendeleo ya nchi.
Pia ameipongeza serikali kwa kuwaona vijana na kuwatengenezea mazingira ya kujiinua kiuchumi kupitia mradi unaolenga kuongeza ushiriki wa vijana katika kilimo kwa kuwapatia mafunzo, maeneo ya mashamba, mitaji na kuwaunganisha na fursa za masoko ( Building a Better Tomorrow-BBT) ambao sasa utawahusisha na vijana wa kujitolea wa JKT ambapo watapata mafunzo katika vituo atamizi.
Amesema tayari Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa  na wizara ya kilimo wameshasaini makubaliano ambapo mpango uliopo sasa ni kurudia yale makubaliano ili kuwahusisha vijana wa JKT katika mpango wa serikali wa kuwa na mashamba nundu.
Aidha amesema hivi karibuni Wizara ya Mifugo na Uvuvi na wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inakwenda kusaini makubaliano ili vijana wanaohudhuria mafunzo ya JKT nao wahusishwe katika mpango huo maalum.
“Ili kuhakikisha mpango unawezeshwa serikali imetoa malekezo kwa taasisi za kibenki kupunguza riba za ukopaji na kutoa masharti nafuu ili wafugaji ,wakulima na wavuvi waweze kuendeleza maeneo hayo ili kuongeza mazao ya chakula,ufugaji na uvuvi na pia itawezesha vijana kupata ajira,itakwenda kuongeza pato la Taifa na uhakika wa usalama wa chakula nchini.
Brigedia Jenerali Mabena amewasihi wananchi wa mkoa wa Mbeya na mikoa ya Jirani kutumia fursa iliyotolewa ya kuingia kwenye maonyesho hayo bila kiingilio kwa kufika hasa katika banda la JKT ambako watapata elimu nzuri ya kilimo,ufugaji na uvuvi kwa lengo la kuwawezesha wananchi kuzalisha kwa tija katika maeneo hayo.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato