November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi wa Kifimbo wamuomba rais Samia kuingilia kati mgogoro wa ardhi

Na David John, TimesMajira Online

WANANCHI wa eneo la Kifimbo katika kijiji cha Muyuyu Kata ya Mtunda wilayani Kibiti mkoani Pwani wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuwasaidia kupata eneo lao la ardhi lenye ukubwa wa ukeri 16,000 ambayo kwa sasa inadaiwa kutolewa kwa muwekezaji huku wao wakiwa hawajui hatma yao.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika eneo hilo la Kifimbo, wananchi hao wamesema wanaishi maeneo hayo kwa zaidi ya 20 sasa na wamekuwa wakijishughulisha na shughuli za kilimo na ufugaji, hivyo wanashangaa kusikia wakiambiwa waondoke huku wakielezwa eneo hilo ni la mwekezaji ambaye ameamua kuchukua eneo lake kwa ajili ya kilimo.

Wakieleza zaidi wananchi hao wamesema wanasikitishwa na hatua ya baadhi ya viongozi wa kijiji kwenda kwenye maeneo yao na kuwapa vitisho kwa lengo la kushinikiza waondoke wakati wao wametumia nguvu zao na fedha kwa ajili ya kufyeka msitu mkubwa ili waendelee na makazi pamoja na shughuli za kilimo na ufugaji.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao kutoka kaya zaidi ya 57 , Kaimu Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyambele Paul Kayamba amesema wako njia panda kwani hawajui hatma yao na kwa nyakati tofauti wamekuwa wakifutuailia suala hilo kwa kwenda viongozi wa Wilaya hiyo akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kibiti na kwamba pamoja na matumaini makubwa waliyonayo kwa Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa wa Pwani bado wanaona kuna kila sababu ya Rais Samia kuingilia kati.

“Ukweli ni kwamba wakati tunakuja maeneo hayo tulifuata taratibu zote ambazo ziliwekwa na Serikali ya Kijiji chetu, tulitoa fedha kwa viwango tofauti kwa kila aliyekuja hapa, wengine nyaraka za kupewa maeneo haya wanazo na wengine zimepotea kwani yalipita mafuruko makubwa yakasomba vitu vyetu muhimu.

“Eneo hili ambalo tumekuwa tukulitumia kwa ajili ya makazi na shughuli za kilimo lina ukubwa wa ekari 16000 na sisi hatuna tatizo na mwekezaji , tunachotaka badala ya kutuondoa basi wagawe , tubaki na ekari 8000 na mwekezaji naye abaki na 8000 kuliko la kutuambia tuondoke na wengi wetu tumetoka bara miaka mingi, hatuna pakwenda.

“amesema kuongeza wanaishi maeneo hayo wakiwa na bibi zao na mama zao, hivyo ni vema Serikali ikawasaidia kutafuta ufumbuzi na wanayo matumaini makubwa na Serikali ya Rais Samia.

Mkazi mwingine wa eneo hilo Mpina Masanja amesema amekuwa eneo kwa zaidi ya miaka sita sasa na anaishi na familia yake akiwemo bibi na mama yake mzazi, hivyo ametoa rai kwa Mkuu wa Wilaya kuwasaidia na bahati nzuri baadhi yao wameshakutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Wilaya.

“Tumekutana na Mkuu wa Wilaya yetu tunamshukuru kwani ameonesha nia njema ya kutusaidia na alitoa maelekezo kwa viongozi walioko chini yake kushughulikia suala hili kupata suluhu ambayo itaridhisha pande zote.”

Ameongeza mgogoro huo umesababisha wengi wao kuishi maisha ya mashaka na kibaya zaidi hawana maeneo ya kulima kwani kote ambako walikuwa wanalima wameambiwa wasilime kwani ni mali ya mwekezaji.

Wakati huo huo mkazi mwingine wa eneo la Kifimbo Merry Mathias mwaka huu kuna uwezekano mkubwa wa kukabiliwa na baa la njaa kwani hadi sasa hawahalima kutokana na changamoto hiyo, hivyo ameiomba Serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma kwani hata famili zao wakiwemo watoto wanasoma kwa fedha wanazopata baada ya kuvuna mazao mashambani.

Naye Geoge Kidawa amesema kinachosikitisha wakati wao wameaambiwa wasilime mashamba yao lakini mwekezaji ameendelea kulima, lakini kwao ombi lao kubwa ni kuona Serikali inatafuta suluhu ili maisha mengine yaendelee huku akieleza kuwa madai ya baadhi ya viongozi wa Serikali ya Kijiji wamekuwa wakidai eneo alilopewa muwekezaji lilikuwa limetengwa kwenye mpango bora wa ardhi.

“Sasa kama eneo hilo lilikuwa limewekwa kwa ajili ya mpango huo kwanini walitukaribisha na kutoa maelekezo yote ambayo tuliyafuata na kwa muda wote tumekuwa tukishiriki shughuli za maendeleo na pale ambapo tulitakiwa kuchangia maendeleo tumefanya hivyo.Tunayo na Shule iliyojengwa na Serikali , hivyo bado tunashangaa kwa haya yanayoendelea,”amesema.

Akizungumzia mgogoro huo, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Muyuyu Hassan Abdallah amesema mengi ambayo yanaelezwa na wananchi wa Kifimbo hayana ukweli wowote na kwamba wameshakaa vikao mara kadhaa na kufikia muafaka huku akiweka wazi hakuna mwananchi ambaye amezuiliwa kulima.

“Katika eneo hilo la Kifimbo tumeshafika viongozi wa ngazi mbalimbali na kufanya vikao, tumezungumza na wananchi na kuwaeleza kuhusu eneo hilo, wamefika mpaka kwa Mkuu wa Wilaya na alishatoa maelekezo.

“Hivyo tulikutana na tukakubaliana na wananchi hao na wale ambao wanataka kulima hakuna aliyezuia kwani mwekezaji mwenye eneo hilo alishasema wanaotaka kulima waendelee kwa kuwa hana nguvu ya kulima eneo lote.Kuhusu kuondolewa tumewaambia hawawezi kuondoka sasa , wataendelea kubaki wakati Serikali ya Kijiji ikiendelea kuwatafutia makazi ya kudumu,”amesema Abdalllah.

Ameongeza kwa bahati mbaya wananchi hao wamekuwa ni watu wa kubadika, wanaweza kuzungumza jambo na wakakubaliana lakini baadae wanageuka na kuzusha mambo mengine, lakini ukweli ni kwamba wengi wao ni wafugaji na hawataki eneo lao liendelezwe kwasababu watakosa maeneo ya malisho na ndio mahitaji yao makubwa

.”Viongozi tutaendelea kuzungumza na wananchi hadi pale tutakapoona wameelewa kuhusu eneo hilo na wanajua ukweli.”