Na Judith Ferdinand, TimesMajira online, Mwanza
Mei 18,2022 serikali inaanza zoezi la utoaji wa chanjo ya polio kwa watoto chini ya umri wa miaka 5,hivyo wananchi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza wameombwa kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo.
Akizungumza na Majira ofisini kwake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Sebastian Pima,amesema,zoezi la utoaji wa chanjo ya polio litafanyika katika vituo vya kutolea huduma pamoja na kutembelea nyumba kwa nyumba.
Hii ni kuhakikisha wanawafikia wananchi wote na kuweza kuchanja watoto ambao wana umri chini ya miaka mitano ambapo kwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza wanatarajia kuchanja watoto takribani 92,000.
Dkt. Pima amesema,zoezi hilo litafanyika kwa siku nne kuanzia Mei 18-21,huku rai yake kwa wananchi wajitokeze lengo ni lile lile kuchanja watoto kuanzia miezi 0 mpaka miezi 59 ambapo watumishi wao, watendaji lakini wenyeviti wa mitaa,wameisha wapa maelekezo na wapo tayari kwa ajili ya kusimamia zoezi hilo.
“Tunawaomba wananchi mjitokeze ili watoto waweze kupata chanjo ya polio ambayo itawasaidia kujikinga na ugonjwa wa kupooza,tunahitaji kutengeneza taifa imara lenye watu wenye afya bora ambao wanaweza wakapambana kuhakikisha uchumi wa nchi unapanda kwa mtu mmoja mmoja na maendeleo ya taifa kwa ujumla,”amesema Dkt.Pima.
Kwa upande wake Mratibu wa chanjo Halmashauri ya Jiji la Mwanza Makubi Gondera, ametoa wito kwa jamii,wazazi na walezi wenye watoto wenye umri chini ya miaka mitano kutoa ushirikiano kwa kuwa tayari kupokea timu za uchanjaji na kupokea chanjo hizo.
Makubi ameeleza kuwa,kwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza wanalenga kuwapatia chanjo watoto 92,698 ambapo kila kitu kipo tayari na zoezi hilo litafanyika nyumba kwa nyumba kila mtaa kutakuwa na timu inayotembea ikiongozwa na Mwenyekiti wa serikali ya mtaa husika.
Ameeleza kuwa,ugonjwa wa polio unaambukizwa kwa njia ya kula na kunywa ambapo unaweza ukanywa maji ambayo yamechafuliwa na kinyesi ambacho kinatokana na mtu ambaye tayari ana kiini cha ugonjwa huo ambapo wadudu hao wanatabia ya kushambilia mifupa ya fahamu na kusababisha mtu kupooza kwa viungo vya mwili.
“Ugonjwa huu hauna dawa isipokuwa una kinga na kinga pekee ni chanjo ambazo tunazitoa kwa watoto wetu wenye umri chini ya miaka mitano na ndio maana tunasisitiza na utafiti umebaini kuwa kundi hili ndio linaathirika zaidi,”amesema Makubi.
Naye Muuguzi wa zahanati ya Nyamagana Julitha Simon, amesema wao kama wauguzi wamejipanga katika zoezi hilo kwanza kwa kubaini maeneo yote ya kutolea huduma kwa kituo chao.
“Tumejipanga kikamilifu kwanza tumefanya zoezi la kutambua maeneo yetu ya kutolea huduma kwa mfano zahanati yetu Ina mitaa minne tumeweza kubaini mitaa yetu minne lakini tumeweza kutoa taarifa tutamfuata kila mama katika mitaa yake naxwatakaoweza kuja kwenye zahanati pia,”amesema Julitha.
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango