January 27, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi Mkolani waitikia wito kampeni ya chanjo ya polio kwa watoto chini ya miaka mitano

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Wananchi wa Kata ya Mkolani wilayani Nyamagana mkoani Mwanza,wamejitokeza kwa wingi katika zoeze la utoaji wa chanjo ya polio kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano huku wakiwahamasisha wengine kuendelea kujitokeza.

Ambapo kampeni hiyo ya utoaji wa chanjo hiyo inafanyika nchi nzima ikiwa na lengo la kuwakinga watoto na ugonjwa wa polio unaosababisha kupooza kwa mwili na viungo vya mwili ilionza leo Mei 18 hadi 21 mwaka 2022.

Wakizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo ambayo kwa Wilaya ya Nyamagana imefanyika zahanati ya Mkolani baadhi ya wananchi hao wamewahimiza wananchi wenzao kuwapeleka watoto wao na kuwa tayari kwa ajili ya zoezi hilo na kuachana na maneno potofu juu ya chanjo hizo kwa watoto.

Mmoja wa wananchi wa Kata hiyo waliojitokeza kupeleka watoto wao katika zahanati hiyo kupata chanjo ya polio,Tunza Hassan amesema,wanaposikia zoezi kama ilo wananchi wakimbilie kupeleka watoto wao kwani usipo mpeleka atakayepata madhara ni mtoto siyo serikali.

“Nimeona bora nimlete mwanangu kwenye chanjo kwa sababu ni haki yake ya msingi,hili ni tamko ambalo ni la taifa na chanjo Ina mkinga mtoto yoyote na maradhi japo kuna baadhi ya jamii zinaona kwamba watoto wataharibika ila ni upotifu wa mtu tu kutokuwa na elimu,”amesema Tunza

Zena Mustapha, amesema chanjo hizo hazina madhara hivyo wazazi wajitokeze kuwapeleka watoto wao ili kuwakinga na maradhi.

“Mimi nina nzao tano na watoto nilikuwa nawapeleka kupata chanjo na mpaka sasa wamekuwa lakini sijawai kuona shida yoyote,wananchi wasikilize serikali na walete watoto kupata chanjo,” amesema Zena.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Jiji la Mwanza Dkt. Sebastian Pima, amesema mwamko wa wananchi katika uzinduzi wa kampeni hiyo walio leta watoto wao kupata chanjo hiyo ni mkubwa pia wameweza kutembelea baadhi ya nyumba katika kata hiyo na kutoa chanjo ya polio.

Dkt.Pima amesema chanjo hiyo haina madhara yoyote na hawategemei mtoto yoyote kupata kitu chochote ambacho siyo cha kawaida baada ya kupata chanjo hivyo wanahamasisha watoto wote waweze kuletwa kwa ajili ya kupata chanjo hiyo.

“Tunamshukuru chanjo hii ya polio imekuwa na mapokeo tofauti na chanjo zingine na mapokeo ni mazuri watoto waliopo ndani ya umri unaotakiwa wazazi wamejitoa kuwaleta kupata chanjo,tutaendelea kutoa chanjo kwa zoezi hili la siku nne na walioipata wahamasishe wenzao wajitokeze ili tuweze kufikia malengo,”amesema Dkt.Pima.

Awali akizindua kampeni hiyo Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi,amewatoa wasiwasi wananchi hao juu ya chanjo hiyo ambapo amesema mwaka 1996 ulipo gundulika ugonjwa huo alikuwa na watoto ambao walipata chanjo ya polio pamoja naye lakini mpaka sasa hajawai kuona madhara yoyote yaliotokana na chanjo hiyo.

Makilagi amesema,hiyo yote ni nia njema ya serikali kwa wananchi wake na hata siku moja haijawai kuwafanyia jambo baya ambapo zoezi hilo limeanza Mei 18 na linatarajiwa kukamilika Mei 21 mwaka 2022 kwa nchi nzima.

Huku lengo la kampeni hiyo kitaifa ni kuhakikisha wanazuia maambukizi ya ugonjwa wa polio nchini kulingana na mlipuko iliotokea huko nchini Malawi na kuongeza kinga kwa watoto wote nchini hapa.

Amesema,ugonjwa wa polio umekuwa tishio kwa miaka mingi kwa nchi nyingi duniani ikiwemo nchi ya Tanzania na mara ya mwisho taifa lilipata mgonjwa wa polio Julai mwaka 1996,hivi karibuni nchini Malawi ilitoa taarifa kuwepo kwa ugonjwa huo Februari 17,2022.

“Kutokana na muingiliano baina ya wananchi wetu na nchi ya Malawi na mataifa mengine, tathimini iliyofanyika na Wizara ya Afya na shirika la Afya Duniani (WHO), nchi yetu ya Tanzania ilionekana ni miongoni mwa mataifa na nchi zilizo katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa polio endapo hatua madhubuti azitachukuliwa,”amesema Makilagi.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi
akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utoaji wa chanjo ya polio kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano ambayo kwa Wilaya ya Nyamagana imefanyika zahanati ya Mkolani.(Picha na Judith Ferdinand)
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Sebastian Pima,
akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utoaji wa chanjo ya polio kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano ambayo kwa Wilaya ya Nyamagana imefanyika zahanati ya Mkolani.(Picha na Judith Ferdinand)
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupeleka watoto wao kupata chanjo ya polio katika uzinduzi wa kampeni ya utoaji wa chanjo ya polio kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano ambayo kwa Wilaya ya Nyamagana imefanyika zahanati ya Mkolani na kuzinduliwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi.(Picha na Judith Ferdinand)
Muhudumu wa afya akimpatia mmoja wa watoto chanjo ya polio inayotolewa kwa njia ya matone wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utoaji wa chanjo ya polio kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano ambayo kwa Wilaya ya Nyamagana imefanyika zahanati ya Mkolani.(Picha na Judith Ferdinand)
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi akimpatia mmoja wa watoto chanjo ya polio inayotolewa kwa njia ya matone wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utoaji wa chanjo ya polio kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano ambayo kwa Wilaya ya Nyamagana imefanyika zahanati ya Mkolani.(Picha na Judith Ferdinand)