Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Korogwe
WANANCHI zaidi 3,684 wa vijiji vya Mgwashi na Kwekibomi katika Kata ya Mgwashi, Tarafa ya Bungu, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga watafaidika na huduma ya maji baada ya mradi wao wa maji kukamilika.
Wataalamu wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) kutoka Makao Makuu pamoja na Wilaya ya Korogwe, walifika kukagua mradi huo Desemba 20, 2022 na kuridhika na mradi huo ambao miundombinu yake imekamilika.
Wataalamu kutoka Makao Makuu ya RUWASA wakiongozwa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa RUWASA Makao Makuu Herieth Kaiza, waliridhika namna mradi huo ulivyotekelezwa, ambapo walifika kwenye vyanzo vya maji viwili (Intake) vinavyopeleka maji Kijiji cha Mgwashi na Kwekibomi.
“Tumeridhika na ujenzi wa mradi ulivyotekelezwa. Tunaamini wananchi wa vijiji hivi watapata maji, na kufikia ile azma ya RUWASA na Serikali ya kuwafikishia maji wananchi kwa umbali usiozidi mita 400” alisema Kaiza.
Kwenye taarifa ya Meneja wa RUWASA Wilaya ya Korogwe Mhandisi William Tupa ilisema, Desemba 29, 2021, RUWASA iliingia mkataba na kampuni ya M/s FHS Engineering Ltd ya mkoani Dar es Salaam kwa ajili ya ujenzi wa Mradi wa Maji wa Mgwashi na Kwekibomi kwa Mkataba wenye Na. AE-102/2021-2022/HQ-C/W/78.
Lengo la mradi huo ni kutoa huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kwa wananchi wapatao 3,684 wa vijiji vya Mgwashi na Kwekibomi.RUWASA Wilaya ya Korogwe ilitengewa kiasi cha sh. milioni 502 kupitia fedha za UVIKO 19 kwa ajili ya utekelezaji mradi wa maji wa Mgwashi na Kwekibomi.
Na RUWASA iliingia mkataba na Kampuni ya FHS Engineering Ltd kwa gharama ya sh. 491,186,632.
“Kazi zilizopangwa kufanyika kwa mujibu wa mkataba ni ujenzi wa banio mbili (2 Intake) katika vijiiji vya Kwekibomi na Mgwashi, ujenzi wa matangi mawili yenye ujazo wa lita 75,000kila moja ambayo yatahudumia vijiji vya Mgwashi na Kwekibomi, ujenzi wa vituo 17 (vilula) vya kutekea maji, kuchimba mtaro, kulaza bomba na kufukia urefu wa mita 14,668, ujenzi wa alama za bomba 165 pamoja na kuzisimika kwenye njia ya bomba, na ujenzi wa chemba 26 ambazo zitajengwa kwenye njia za bomba.”
“Kazi zilizofanyika hadi kufikia Novemba 30, 2022 ni ujenzi wa kingamaji (intake) katika Kijiji cha Mgwashi umekamilika kwa asilimia 100, ujenzi wa kingamaji (intake) katika Kijiji cha Kwekibomi umekamilika kwa asilimia 100, ujenzi wa tanki la lita 75,000 katika Kijiji cha Mgwashi umekamilika kwa asilimia 100, ujenzi wa tanki la lita 75,000 katika Kijiji cha Kwekibomi umekamilika kwa asilimia 100” ilisema taarifa hiyo.
Kazi nyingine zilizofanyika ni kuchimba mtaro na kulaza bomba pamoja na kufukia urefu wa mita 13,840 umekamilika kwa asilimia 100, ujenzi wa vituo 17 (vilula) katika vijiji vya Mgwashi vilula 10 na Kwekibomi vilula saba, na ujenzi umekamilika, ujenzi wa alama za bomba 165 kwenye njia ya bomba umekamilika, na ujenzi wa chemba 26 kwenye njia za bomba na kona zake zimejengwa kwa asilimia 99.
Kwa mujibu wa mkataba, mradi huo ni wa miezi sita na ulianza kutekelezwa Januari 24, 2022 na ulitarajiwa kukamilika Julai 24, 2022, lakini kutokana na changamoto mbalimbali, Mkandrasi aliomba kuongezewa muda wa siku 135 katika kipindi tofauti tofauti na RUWASA ikaridhia na kumpa muda huo ambao uliisha Novemba 30, 2022, na sasa mradi umekamilika.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi