Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Korogwe
WANANCHI wa Kijiji cha Kwetonge, Kata ya Mashewa, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, wamekitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutekeleza ahadi zake zilizopo kwenye Ilani ya CCM ya 2020- 2025, ya kuwapatia maji.Waliyasema hayo kwa nyakati tofauti Februari 4, 2023 katikati ya sherehe za miaka 46 ya kuzaliwa chama hicho zilizofanyika kiwilaya Kijiji cha Kwetongo, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Korogwe Vijijini Ally Waziri.
“Tangu tupate Uhuru kijiji chetu cha Kwetonge hakijapata maji ya bomba. Na hata zahanati yetu mpya ambayo imejengwa na Serikali huku wananchi wakichangia nguvu zao, haitaweza kufanya shughuli yeyote kwa vile hakuna maji.”
“Awali Serikali ilichimba maji ya kisima kirefu, lakini maji yake yakawa mabaya yana chumvi, na sasa imechimba kisima kingine maji mazuri yamepatikana, lakini maji hayo bado yapo ardhini, hayajajengewa miundombinu. Hivyo tunaomba Serikali iweze kutupatia maji” alisema Lucy Kisia mkazi wa Kijiji cha Kwetonge.
Naye Fatuma Kaghambe ambaye ni Mwenyekiti wa UWT Tawi la Kwetonge alisema wanawake wa kijiji hicho wanateswa na maji tangu Uhuru, hivyo wanaiomba CCM kuweza kuweka msisitizo kwa wataalamu wa maji kuweza kuwawekea maji ya bomba.Naye Nuru Ukoko ambaye ni Katibu wa CCM Tawi la Kwetonge alisema, tayari Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilaya ya Korogwe, wameshachimba kisima kirefu kwa mara ya pili, na wamepata maji baridi na yanafaa kwa matumizi ya binadamu, hivyo wanataka mchakato wa kujenga miundombinu ya maji uharakishwe.
“Dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kumtua ndoo kichwani mwanamke wa kijijini. Tunawataka wataalamu wa maji waweze kuja kuweka miundombinu ya maji ili kutimiza azma ya Mama Samia kwa wananchi kupata maji” alisema Ukoko.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Korogwe, Waziri, alimtaka Mhandisi wa RUWASA Wilaya ya Korogwe Joyce Malekela ambaye alikuwepo kwenye mkutano huo, atoe maelezo juu kero hiyo ya maji, ambapo alisema ni kweli wamechimba kisima kirefu cha maji kwenye kijiji hicho, na nia ni kujenga mradi wa maji kwa kuweka miundombinu.
“Ni kweli Kwetonge wana shida ya maji, lakini tayari RUWASA tumeanza mchakato wa kujenga mradi wa maji, ambapo tayari kisima kirefu kimechimbwa, na maji yamepatikana. Sasa tupo kwenye hatua za manunuzi, na mchakato huo unakamilika mwezi huu wa Februari, na ujenzi kuanza, na mradi utakamilika ndani ya miezi sita.”
“Mradi huo wa sh. milioni 600, utajengwa tenki lenye ukubwa wa lita 100,000, na kuwekwa vituo vya kuchotea maji (vilula) 11, huku maji hayo yakiwekwa kwenye taasisi za Serikali ikiwemo Zahanati ya Kijiji cha Kwetonge” alisema Malekela.
Waziri alisema, kupeleka fedha za miradi ni jambo moja, kutekeleza mradi ni jambo jingine, na kulinda miradi ni jambo jingine. Hivyo ametaka kuhakikisha fedha zinazotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zifanye kazi zilizokusudiwa kwa weledi.
Alisema baada ya mradi kukamilika, ni lazima wananchi wachangie huduma hiyo ya maji kwa kulipia, huku wao wananchi ndiyo wakiwa walinzi wa mradi huo kwa kuhakikisha miundombinu ya maji inalindwa.
“Msitumie maji hayo bure, na ni lazima mlipie maji hayo ili mradi uwe endelevu. Rais ameshatoa fedha za kuweza ninyi kupata maji, hivyo haiwezekani alete na fedha za kufanyia matengenezo ya mradi kwa vile Tanzania hii ni kubwa, kwani Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe yenyewe ina kata 29, vijiji 118 na vitongoji 610 . Na fedha za maji zisomwe kwa wakati ili wananchi waone fedha zao zipo salama.”
“Tuhakikishe tunalinda miundombinu ya maji kuona inakuwa endelevu. Asije akatokea mwananchi kuhujumu miundombinu au kukataa kuchangia maji, labda huyo mtu akaishi hewani, lakin sio hapa kijijini. Tunataka ushirikiano kuona miradi ya maji inakuwa endelevu, na wananchi wanaondokana na shida ya maji” alisema Waziri.
Waziri alisema miradi mingi ya maji imetekekezwa kipindi cha Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia, hivyo lazima miradi hiyo wailinde sababu ni ya fedha nyingi, huku akiwamwagia sifa Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo, na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Korogwe Mhandisi William Tupa.
“Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Korogwe ndugu yangu Tupa pamoja na wataalamu wa RUWASA, hawa wanafanya kazi kubwa na nzuri. Ukiangalia miradi iliyojengwa na inayoendelea kujengwa ukiwemo wa Mgwashi- Kwekibomi, Kwemasimba, Mombo- Mlembule, Sekioga, Makuyuni na Magila- Gereza, utaona imejengwa kwa kiwango” alisema Waziri.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato