January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi Ludewa wapatiwa mizinga ya nyuki 300

Na Mwandishi wetu,timesmajira, Online

Wizara ya Maliasili na Utalii imekabidhi mizinga 300 kwa vikundi mbalimbali vilivyoundwa na wananchi wilayani Ludewa mkoani Njombe kama sehemu ya kuwajengea uwezo wa kiuchumi wananchi hao.

Akigawa mizinga hiyo Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana amesema moja ya wajibu wa Wizara anayoiongoza ni kushirikiana na wanachi ambao ndio wadau wa kwanza katika uhifadhi endelevu.

Amesema Wizara imeona ipo haja ya kuwapatia wananchi hao Mizinga watakayoitumia kama chanzo cha mapato pia kuimarisha ulinzi katika hifadhi za Misitu.

Waziri Chana amewataka wananchi waliopata mizinga hiyo na mafunzo ya ufugaji nyuki kuitunza na kuwaelimisha wengine juu ya faida ya Misitu hasa ufugaji Nyuki, hasara inayotokana na uharibifu wa Misitu pamoja na adhabu ambazo zimeainishwa kisheria ikiwemo hukumu ya kifungo cha miaka 15 kwa yeyote atakaebainika kuchoma moto misitu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kata ya Ludende, Mariam Mdege amesama mafunzo na mizinga waliyopatiwa licha ya kuimarisha mahusiano bora kati ya wananchi na Serikali itachochea ukuaji wa uchumi kwa jamii huku akiishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwawezesha .