Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Rungwe
WANANCHI wa Kata ya Kisondela wilayani Rungwe mkoani Mbeya wameishukuru serikali kwa ujenzi wa Shule mpya ya Ufundi ya Amali iliyopo kwenye kata hiyo na kusema kuwa imeongeza ajira pamoja na kuchavusha uchumi kwa watumishi na wanafunzi wa shule hiyo katika kunufaika na bidhaa za kilimo zinazopatikana kwenye eneo hilo .
Wamesema hayo leo Januari 9,2024 wakati Mkuu wa wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya,Jaffar Haniu alipofanya ziara na kukagua na hatua za ujenzi wa shule ya Amali ya Ufundi iliyopo kwenye kata hiyo.
Amanyisye Kalinga ni mkazi wa Mpugha kata ya kisondela amesema kuwa kufuatia uwepo wa ujenzi huo kumekuwa mabadiliko makubwa ya kiuchumi katika eneo hilo ambalo wakazi wake wanajishughulisha na kilimo.
Haniu pamoja na mambo mengine ameridhishwa na hatua ya ujenzi iliyofikiwa na kuwa hii itasaidia ukuaji wa maarifa na ujuzi kwa wakazi wa wilaya ya Rungwe pindi ujenzi utakapokamilika.
Aidha Haniu ameagiza mafundi wanaotekeleza mradi huo kufanya kazi usiku na mchana ili kusaidia ukamilishaji wa ujenzi wa shule hiyo kwa wakati.
“Ndugu zangu hakikisheni ujenzi huu unakamilika kwa wakati ili Shule hii iweze kuanza mapema na watoto wetu waweze kuanza masomo yao mapema”amesema Mkuu huyo wa Wilaya.
Jumla ya Shilingi Million 583 zimetolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo ambapo Baraza la Madiwani tayari limetoa azimio la kusajiliwa kwa jina la Renatus Mchau mara baada ya ujenzi wake utakapokamilika.
Kata ya Kisondela ni maarufu kwa kilimo cha ndizi, parachichi,machungwa, mahindi na karanga ambapo kimekuwa kilimo maarufu kwa kuwaingizia kipato wananchi.
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango
LALJI yatoa msaada wa sare na vifaa vya shule kwa yatima