Na Heri Shaaban, TimesMajira Online
MBUNGE wa Jimbo la Segerea, Bonnah Ladslaus Kamoli, amewahakikishia wananchi wa Kipunguni kuwa Serikali inaendelea na michakato ya ulipaji fidia na kuwataka waendelee kuwa wavumilivu.
Wananchi hao wanaotakiwa kupisha Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere wanatakiwa kulipwa fidia hizo ambazo wamesubiri kwa muda mrefu tangu walipofanyiwa tathmini.
Mbunge Bonnah Ladslaus Kamoli, alisema hayo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Kipawa wilayani Ilala wakati akielezea utekelezaji wa Ilani uliofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mbunge Bonnah alisema mchakato wa fidia Kipunguni ulianza tangu mwaka 1997 na mpaka sasa wananchi hao waliambiwa wasiendeleze ujenzi wowote kwa ajili ya upanuzi wa uwanja wa Ndege wa kisasa.
“Wananchi wametii agizo la Serikali wanasubiri wapewe haki yao, mchakato wa kuwalipa unaendelea serikalini, nawaomba muwe wavumilivu mimi niko na ninyi mpaka mpate haki yenu,” amesema Bonnah.
Akizungumzia mafanikio ya Kata ya Kipawa amesema maboresho makubwa yamefanywa katika sekta ya elimu na afya na kwamba baadhi ya barabara tayari zimeingizwa katika Mradi wa DMDP kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami na zege.
Akizungumzia mikopo ya vikundi alisema wakopaji wengi kutoka Kipawa walifanikiwa kupata na kushauri itakapoanza kitolewa tena wanawake wa hali ya chini ambao hawahitaji fedha nyingi wapewe kipaumbele.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Kipunguni, Mwijuma Seke, alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa utekelezaji wa Ilani ya chama vizuri katika mtaa huo.
Amesema Rais Samia amefanya mambo makubwa amejenga shule ya sekondari ya kisasa sekondari ya Minazi Mirefu ambayo itawekwa lifti.
Alisema pia Barabara ya Banana Kitunda inatarajia kujengwa kupitia Mradi wa Kuboresha Miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP) na kwamba zote hizo ni juhudi za Mbunge Bonnah Kamoli na Rais Dkt. Samia.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kipawa, Said Mkuwa, aliipongeza Serikali ya Dkt. Samia kwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho ambapo katika Kata ya Kipawa wanajivunia kuwa na shule nane za msingi na tatu za sekondari pamoja na sekta ya afya.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa