November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi Igunga kuanza kunufaika mtambo wa kutibu maji taka

Na Lubango Mleka, TimesMajira Online – Igunga.

WANANCHI wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Igunga na maeneo ya jirani na wilaya ya Igunga kuanza kunufaika na matumizi ya Mtambo wa kutibu Majitaka na Topetaka ifikapo mwishoni mwa mwezi Octoba, 2024.

Hatua hii ni kukabiliana na kuepukana na magonjwa ya mlipuko ya kuambukizwa yanayotokana na kusambaa kwa taka na maji katika maeno mbalimbali ya halmashauri hii.

Akitoa taarifa mbele ya Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Igunga, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (IGUWASA) Mhandisi Humphrey Mwiyombela amesema kuwa, ujenzi wa mtambo huo ulianza mwezi Julai 2023 unatarajia kukamilika Octoba mwaka huu.

” Pamoja na jukumu la kusambaza maji Safi na Salama ya kunywa mjini Igunga, IGUWASA tuna jukumu jingine la kuhakikisha kuwa mazingira yanakuwa safi na salama, ” amesema Mhandisi Mwiyombela.

Ameendelea kusema kuwa katika kuhakikisha mji wa Igunga unakuwa safi, Mamlaka hiyo inatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa mtambo wa kusafisha majitaka na topetaka unagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 1.8 fedha kutoka Serikalini.

Mhandisi Mwiyombela anasema, mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 23 na kukamilika kwake kutawanufaisha jumla ya wakazi 82, 768 katika vitongoji vya mji wa Igunga na wilaya za jirani.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Igunga, Mafunda Temanya akisema kuwa mradi huo ni muhimu kwa ustawi wa afya ya wananchi wa Igunga na maeneo ya jirani na wilaya hii, hivyo amewataka IGUWASA kuhakikisha wanamsimamia Mkandarasi vizuri ili amalize mradi kwa wakati.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Igunga Mjini (IGUWASA) Mhandisi Hamphrey Mwiyombela (mwenye shati la rangi ya bluu bahari) akitoa maelezo juu ya hatua ya awali ya ujenzi wa miundombinu ya kutibu majitaka na topetaka kwa kamiti ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Igunga walipotembelea kukagua mradi huo.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Igunga Mafunda Ntemanya wa kwanza kushoto akiwa na wajumbe wa kamati ya Siasa wa Chama hicho wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Igunga Mjini (IGUWASA) hayupo pichani alipokuwa akitoa taarifa ya ujenzi wa mtambo wa kusafisha majitaka na topetaka unaotarajiwa kukamilika Octoba, 2024.