December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi 4,543 Magila-Gereza wanufaika na mradi wa maji

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe

MRADI wa Maji Kata ya Magila- Gereza katika Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga umekuwa mkombozi kwa wananchi 4,543 wa vijiji vitatu vya kata hiyo, kwani tangu nchi kupata Uhuru, wananchi hao hawajawahi kutumia maji ya bomba.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi, wananchi hao walimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake, kwani ameleta mageuzi makubwa kwenye huduma za jamii ikiwemo maji, elimu, afya na barabara

Diwani wa Kata ya Magila- Gereza Mwajuma Kitumpa amesema mradi huo umenufaisha wananchi wa vijiji vitatu vya Magila- Gereza, Mkobe na Kalekwa, huku vitongoji vyake pia vikipata maji hayo.

“Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa makubwa aliyotufanyia hasa sisi wananchi wa Kata ya Magila- Gereza, kwani tangu nchi kupata Uhuru, hatujawahi kutumia maji ya bomba, lakini katika kipindi hiki kifupi cha miaka mitatu, tumeweza kupata mradi wa maji wa sh. 775,743,809.

“Kwangu mradi huu umekuwa ni mkombozi sana kwa wananchi wangu, kwani ukiwa umefikia zaidi ya asilimia 90, unatoa maji,jambo hili ni kubwa sababu wananchi walikuwa wanatafuta maji kutoka maeneo ya mbali, huku wakiwa hawana uhakika wa kuyapata.

“Ndoa zilikuwa zinatetereka sababu mwanamke alikuwa anachukua masaa mengi kutafuta maji kwenye milima,”amesema Kitumpa.

Mwananchi Monica Mwakidungwe wa Kijiji cha Kalekwa amesema sasa hivi wamepata utulivu, kwani wana uwezo wa kwenda shamba alfajiri, na wanaporudi wana uhakika maji watachota nyumbani bila kwenda mbali.

Naye Lucas Kimako mwananchi wa Kijiji cha Magila- Gereza amesema walikuwa wanahatarisha maisha yao kwa kuchota maji mtoni, kwani mamba walikuwa ni tishio, hivyo wanamshukuru Diwani wa Kata ya Magila- Gereza Kitumpa, Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini Timotheo Mnzava na Rais Dkt. Samia.

Mwenyekiti wa CCM Kata ya Magila Gereza Yahaya Mandia amesema Rais Dkt. Samia ameweza kufanya mambo mengi kwa wananchi ikiwemo kuimarisha huduma za kijamii kama maji, umeme na shule, hivyo wataendelea kumsaidia kwa kuona anaendelea kutekeleza Ilani ya CCM 2020- 2025.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Magila- Gereza George Singano amesema maji waliyokuwa wanatumia wananchi yalikuwa yanatoka Mashindei, hivyo watu wanaolima huko wakipiga dawa kwenye mazao yao, wanafanya watu wa Kalekwa wakitumia maji hayo, wanapata magonjwa ya kuhara, hivyo maji hayo ya bomba ni muhimu.

Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Korogwe Mhandisi William Tupa amesema tenki la mradi huo lina ujazo wa lita 300,000, bomba za kutoa maji kutoka kwenye chanzo hadi tenki ni kilomita 5,040, na bomba la kusambaza ni kilomita 28. Pia utakuwa na vilula (DP) 28.