January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanamuziki zaidi ya 100 wajitokeza kuwania tuzo

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limesema kuwa hadi kufikia jana jumla ya wanamuziki zaidi ya 100 wamefungua akaunti kwenye mfumo Kwa ajili ya kuwasilisha kazi zao kupitia mfumo.

Pia jumla ya kazi zaidi ya 90 zimewasilishwa kupitia mfumo.

Hii ni baada ya kutangaza rasmi vipengele vya Tuzo na Mfumo wa Uwasilishaji wa kazi zitakazowania Tuzo kwa mwaka 2021.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mtendaji kutoka BASATA, Matiko Mniko alisema BASATA wanaendelea na jitihada mbalimbali za kuhamasisha wanamuziki kushiriki katika tuzo hizo.

“Kuna jitihada mbalimbali za kuhamasisha ushiriki wa wanamuziki katika tuzo hizi na katika kukamilisha azma hiyo wawakilishi wa baraza watafanya ziara maalum katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Arusha, Mbeya, Mwanza na Zanzibar.
Nia ya ziara hii ni uhamasishaji wa wanamuziki kushiiriki katika Tuzo, ” alisema.

Aidha Mniko alisema muitiko wa wanamuziki ni mzuri na napenda kuwatangazia kuwa kuna wanamuziki wenye hadhi kubwa na wazoefu tayari wameonyesha nia ya kuwania tuzo na kuwasilisha kazi zao.

Pia Mniko aliendelea kusisitiza juu ya mfumo wa uwasilishaji wa kazi ambazo zitashiriki katika tuzo hizo kwamba ni rafiki na rahisi kwenye matumizi.

“Mfumo wa uwasilishaji wa kazi zitakazoshiriki katika Tuzo ni rafiki na rahisi kuutumia na pia Baraza litaendelea kutoa elimu na msaada mtandaoni (online support) wa jinsi ya kutumia mfumo huo wakati wote wa zoezi la uwasilishaji wa kazi za muziki zitakazowasilishwa kuwania Tuzo.” alisema.

Kaimu Katibu Mtendaji huyo aliongeza kuwa kila mwanamuziki atatakiwa kujisajili kwenye mfumo na kuwasilisha kazi husika.

Mniko alisema zoezi la ukusanyaji wa kazi linafanyika kwa siku kumi na nne (14) kuanzia Februari 9, 2022 hadi 22 saa sita (6) usiku. Kazi zitakazokusanywa ndizo zitakazoshiriki katika kuwania Tuzo za Muziki Tanzania kwa mwaka 2021 na si vinginevyo.

Mbali na hayo Mniko alitoa wito kwa wanamuziki wote katika ushiriki wa tuzo hizo.

“Napenda kutoa wito kwa wanamuziki wote nchini kushiriki katika tuzo kupitia mfumo tajwa hapo juu na kama kutakuwa na changamoto ya kimfumo kuna nafasi ya mawasiiliano ya ana kwa ana kwa afisa wa BASATA kupitia Mfumo.” Alisema.