November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanamtandao washerehekea ushindi safari ya vita rushwa ya ngono nchini

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

WANAMTANDAO wa Harakati za Kupambana Dhidi ya Rushwa ya Ngono wamesherekea na kutafakari ushindi walioupata juzi Bungeni baada ya kukataliwa kwa mabadiliko ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Ngono.

Wamesherehekea ushindi huo baada ya kifungu cha 25 kilichopendekezwa kuondolewa na badala yake kuwekwa kifungu kidogo cha 10 (b) kilichodhamiria kumhukumu mhanga wa rushwa ya ngono.

Akizungumza kwa niaba ya mtandao huo jana Jijini Dar es Salaama, Mkurugenzi wa Ruzuku kwa Wanawake Tanzania (WFTT) Rose Marando, alisema wanatambua mchango mkubwa uliofanywa na Chama cha Wanawake Majaji ambao waliwezesha kuingizwa katika sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa kifungu cha 25 kilichotofautisha rushwa ya ngono na rushwa zingine.

“Kwa kuzingatia maamuzi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yaliyofanyika siku ya jana (juz Septemba 2, mwaka huu), ambapo Serikali iliazimia kukabiliana na mapendekezo ya kamati ya Bunge ambayo yamekuwa msimamo wa Mtandao wetu pia na kufuta kifungu 10 (b) na kuacha kama kilivyo kifungu cha 25 cha Sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa ya ngono, 2007 no. 11.,” alisema Marando na kuongeza;

” Pia, Bunge lilienda mbali zaidi na kuongeza wigo wa ukomo wa adhabu kwa waomba rushwa ya ngono kutoka miaka mitatu hadi 10 na faini sh. milioni 5 hadi Mil. 10.”

Alizidi kuongeza kwamba; “Sisi wanamtandao wa kupambana na rushwa tunapenda kuchukua fursa hii kupongeza wanamtandao wote kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania, waandishi wa habari, wadau wa kimataifa waliotuunga mkono na jamii ya Watanzania kwa kusimamama kidete kupaza sauti zao na kukataa mapendekezo ya kifungu 10 (b) kilichotaka mhanga wa rushwa ya ngono kushtakiwa kama mhalifu.”

Alisema hatua ya Bunge kuridhia kutopitisba kifungu hicho na kuongeza adhabu kwa waomba rushwa ya ngono ni ushindi mkubwa kwenye mapambano dhidi ya rushwa ya ngono na uthibitishi tosha wa nguvu ya wananchi na umuhimu wa sauti zao kama wanajamii katika kukataa mifumo kandamizi.

Aidha, alieleza kwamba rushwa ya ngono inaathari nyingi kwa mhanga ikiwemo kumongonyoa na kudhalilisha utu wake, kumnyima fursa za kukuza vipaji vyake, kufanya awe mtumwa wa ngono na kutoa nafasi za upendeleo kwa asuye na sifa stahiki.

“Kwa kuzingatia matokeo ya tafiti zilizofanywa na TAKUKURU kwa kushirikiana na wana mtandao wanaopinga rushwa ya ngono, tunatambua ukubwa wa tatizo hili kwenye jamii yetu ikiwa ni pamoja na majumbani, watumishi wa kazi za nyumbani wakiwa wahanga wakuu, mashuleni kwenye maeneo mengi ya utumishi wa umma na binafsi, maeneo ya biashara, kwenye hospitali zetu hasa kwa wagonjwa wa kike na hata kwenye taasisi za dini.

Hata hivyo wana mtandao hao wametoa pongezi kwa kamati ya utawala Katiba na Sheria kwa kutumia wajibu wao kwa kuishauri Serikali kutopitisha kifungu hicho.

“Tunapenda kuipongeza Kamati ya Utawala , Katiba ya Sheria kwa kutimiza wajibu wake vizuri na kuishauri Serikali kutopitisha kifungu hicho.

Pia wabunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutimiza wajubu wao kikamilifu kwa mujibu wa Katiba yetu na kuweka maslahi mapana ya wananchi mbele” alisema.