November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanahabari waelimishwa matumizi ya Takwimu za Sensa

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Shinyanga

ZAIDI ya wanahabari 100 kutoka Mikoa ya Geita, Simiyu, Shinyanga na Tabora wamepewa mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya takwimu za sensa ya watu na makazi iliyofanyika nchini mwezi Agosti 2022.

Mafunzo hayo ya siku 2 yaliyoandaliwa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) yanafanyika leo na kesho katika ukumbi wa hoteli ya Karena mjini Shinyanga.

Akifungua mafunzo hayo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme amesema mafunzo hayo ni muhimu sana kwa kuwa yatawapa wanahabari uelewa wa kina wa matokeo hayo na kuyatumia kuhabarisha umma.

Amempongeza Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Anna Makinda kwa kusimamia vizuri zoezi hilo na kupata mafanikio makubwa.

Amebainisha kuwa matokeo ya takwimu za sensa ya watu na makazi yatasaidia sana kuchochea kasi ya maendeleo miongoni mwa jamii.

RC Mndeme amefafanua kuwa sekta ya habari ina mchango mkubwa sana katika kufikisha matokeo hayo kwa wananchi hivyo akatoa wito kwa idara na taasisi mbalimbali kuwapa ushirikiano watakapohitaji takwimu zinazohusiana na matokeo hayo ili kufanikisha makujukumu yao.

Naye Kamisaa wa Sensa Anna Makinda amesema mafanikio ya zoezi hilo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ushiriki wa vyombo vya habari kuanzia mwanzo hadi mwisho.

‘Nawapongeza wanahabari wa vyombo vyote kwa kushiriki ipasavyo kuhamasisha jamii kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo, mmetusaidia sana kufanikisha zoezi hilo,’ amesema.

Amefafanua kuwa mafunzo hayo yatawapa fursa ya kujua namna ya kupata takwimu za matokeo hayo kupitia mitandao na kuzitumia katika taarifa zao.

Aidha ameongeza kuwa baada ya mafunzo hayo wanahabari wataweza kusambaza matokeo ya takwimu hizo na kuzitumia katika vyombo vyao ili kuleta tija kwa jamii.

Akiongea kwa niaba ya wanahabari, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga Greyson Kakuru ameishukuru NBS kwa kuwapa mafunzo hayo kwani yatawasaidia kujua namna ya kupata takwimu sahihi za matokeo ya sensa hiyo.

Ameomba Maafisa wa Taasisi mbalimbali za umma kutoa ushirikiano kwa wanahabari watakapohitaji takwimu zinazohusiana na idara zao ili kukamilisha habari zao.

Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi nchini Anna Semamba Makinda akiongea na wanahabari zaidi ya 100 kutoka Mikoa ya Geita, Simiyu, Shinyanga na Tabora.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme akifurahia jambo mbele ya wanahabari alipokuwa akifungua mafunzo yao ya siku 2.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Kamisaa wa Sensa Anna Makinda (kushito) na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Johari Samizi (kulia) wakati wa mafunzo ya waandishi wa habari kutoka Mikoa ya Geita, Simiyu, Shinyanga na Tabora.
Baadhi ya wanahabari wakifuatilia mafunzo ya siku 2 ya usambazaji na utumiaji na matokeo ya takwimu za sensa ya watu na makazi.