Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Onine, Zanzibar
WANAWAKE wana uwezo wa kushika nyadhifa mbalimbali katika vyombo vya habari ili haki na usawa wa jinsia uweze kupatikana katika hivyo.
Akizungumza katika siku ya kwanza ya mafunzo ya siku nne kuhusu wanawake na uongozi katika vyombo vya habari mjini Zanzibar jana, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga, amesema kuwa mafunzo hayo yana lengo la kutoa mwanga kwa wanawake walio katika nafasi mbalimbali ili kuongeza ujuzi wao.
Amesema kuwa suala la usawa wa jinsia hususan katika nyadhifa katika vyombo vya habari bado lipo chini na wanaume wanakuwa ndio wenye kupata nafasi zaidi katika kuongoza vyombo vya habari.
“Tafiti zilizofanywa zinaelezea kuwa wanawake bado ni wachache katika nafasi za uongozi katika vyombo vya habari hivyo juhudi zaidi zinahitajika ili jinsia zote ziweze kupata haki sawa katika uongozi”, ameongeza.
Amesema kuwa ingawa tafiti zinaonyesha kuwa wanawake wanakuwa wengi zaidi katika vyuo vya habari lakini katika vyombo vya habari ni wachache wanaopata nafasi.
“Mafunzo haya ya siku nne yatakuwa ni dira kwa wanawake walio wabobevu na ambao wanashika nyadhifa mbalimbali katika vyombo vya habari kupata weledi na umahiri wa uongozi katika vyombo vya habari”, amefafanua
Mwezeshaji Pili Mtambalike amesema kuwa katika wakati huu ambao kuna mabadiliko makubwa katika masuala ya habari ni lazima viongozi wawe wabunifu katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Wakati huu ambao kuna vyombo vya habari vya asili na vile vya mitandao ya kijamii viongozi hawana budi kutumia vyombo vyote katika kupeleka ujumbe wao huku wakizingatia weledi na umahiri katika kutekeleza majukumu hayo alifafanua.
Amesema kuwa uongozi ni dhamana hivyo dhamana hiyo haina budi kuwa na dhima juu yake ili kuweza kuwanyanyua wale dhaifu na kuimarisha wale ambao wana ujuzi na umahiri katika utekelezaji wa kazi zao za kila siku.
Naye Meneja wa Fedha wa MCT, Mustafa Peter, amesema ni muhimu kufahamu taratibu za maasula ya fedha na kama kiongozi ili waweze kufanikisha kazi zao kwa ufanisi.
“Suala la fedha ni muhimu katika kazi za kila siku hivyo kufahamu taratibu na kuzifuata ili ufanisi wa kazi uweze kupatikana”, amefafanua.
Amesema kuwa mara nyingi viongozi huwa hawataki kufuatilia taratibu za fedha na kusema kuwa wao sio wahasibu hilo ni kosa taratibu za fedha zifahamike kwa uwazi kwani uongozi na masuala ya fedha ni mambo yanayokwenda kwa pamoja
Naye Meneja Rasilmali Watu na Utawala wa Baraza, Ziada kilobo amesema mafunzo hayo ya siku nne ni mojawapo ya hatua za kuimarisha usawa na haki ya uongozi katika vyombo vya habari.
Amesema kuwa hii ni mara ya nne kwa MCT kuandaa mafunzo kama hayo na tayari wanawake viongozi 61 wamepata mafunzo hayo na yataendelea hadi mwaka 2024 kwa awamu mbalimbali.
Mafunzo hayo ambayo yanaratibiwa na kwa ufadhili la Shirika la VIKES la Finland ambapo kazi mbalimbali zitaendelea kwa lengo la kuimarisha haki na usawa wa jinsia katika vyombo vya habari.
Mafunzo hayo ya siku nne yamewashirikisha wanahabari wanawake 15 walioko katika nyadhifa mbalimbali katika sehemu mbalimbali Tanzania na yanafanyika Zanzibar.
More Stories
Wanaoficha watoto wenye ulemavu kusakwa
Mawakili Tabora walaani kuziwa kutekeleza majukumu
RC Mrindoko:Ufyekaji wa mahindi Tanganyika si maelekezo ya serikali