January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanahabari, Oryx kumuunga mkono Samia matumizi ya nishati safi

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

WIKI iliyopita Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwenye ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa 13 wa kitaaluma uliofanyika Dodoma, ukiwa na kauli mbiu isemayo;

“Uandishi wa Habari Kuhamasisha Matumizi ya Gesi Kulinda Misitu.”

Kauli Mbiu hiyo ilibeba ujumbe unaozingatia kwamba Rais Samia Suluhu Hassan, Novemba mwaka jana, amechaguliwa kuwa Kinara (Champion) wa Ajenda ya Nishati Safi na Salama ya Kupikia kwa Wanawake wa Afrika katika mkutano wa COP28 uliofanyika nchini Dubai.

Kwa kutambua hilo, TEF iliona ni bora vyombo vya habari navyo vishiriki kuunga mkono nia hiyo njema ya Rais Samia na hasa kwa kutambua kwamba suala muhimu.

Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, anasema wakati wakitafakari nafasi ya kaulimbiu hiyo, walibaini kuwapo kwa dalili za rasilimali ya gesi kutotumika ipasavyo kutatua changamoto hasa katika sekta ya nishati, kwa maana ya upatikanaji wa umeme nchini na kutumiwa kama nishati safi ya kupikia kwa akina mama, licha ya kujengwa bomba la kusafirisha rasilimali hiyo kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, ambalo ujenzi wake uligharimu mabilioni ya shilingi za Kitanzania.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile, akizungumza kwenye mkutano wa 13 wa kitaaluma uliofanyika Dodoma, ukiwa na kauli mbiu isemayo;
“Uandishi wa Habari Kuhamasisha Matumizi ya Gesi Kulinda Misitu

“Bomba hili kwa taarifa tulizonazo linatumika kwa kiwango cha chini kwani miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi pale Kenyerezi, Dar es Salaam haijafanya kazi kwa idadi ya megawati zilizokusudiwa. Tuliahidiwa Kinyerezi I, II, III na IV, lakini taarifa tulizonazo, Kinyerezi III na IV hazijafanya kazi kwa kiwango kilichokusudiwa,” anasema.

“Sisi Wahariri, tunatamani kuona mchango wa rasilimali gesi katika uchumi wa nchi yetu na watu wake, na zaidi kusaidia taifa kuondokana na changamoto ya akina mama wenye macho mekundu kutokana na moshi wa kuni kudhaniwa kuwa ni wachawi na kuuawa katika baadhi ya mikoa hapa nchini.

Mgeni rasmi kwenye mkutano huo, Naibu Waziri Doto Biteko, anasema amefurahishwa na kaulimbiu ya mkutano huu ambayo ya Uandishi wa Habari Kuhamasisha Matumizi ya Gesi Kulinda Misitu.

“Nyote mnafahamu kuwa dunia imemchagua Rais Samia kuwa Kinara wa uhamasishaji matumizi ya Nishati safi ya kupikia, ambayo ni gesi kwa Bara la Afrika.

Kwa mabara mengine kama Ulaya, Amerika ya Kusini na Kaskazini na Asia, kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia nishati ya gesi kwa ajili ya kupikia majumbani.

Kwa mabara haya, kukata mti kwa ajili ya kuni au mkaa inachukuliwa kuwa ni uhalifu usiokubalika,” anasema Dkt. Biteko.

“Wenzetu wanatumia gesi kwa ajili ya kupikia, mfumo wa joto katika nyumba zao katika kipindi cha majira ya baridi, na kama Mwenyekiti alivyosema, gesi inatumika sasa kuendeshea magari. Sisi kama Wizara ya Nishati tumeandaa mpango kabambe wa kuhamasisha matumizi ya gesi hapa nchini.

Wakati Rais wetu, Mama Samia anakwenda katika nchi nyingine za Afrika kuhamasisha matumizi ya gesi, sisi tumesema nchi hizo zije kujifunza hapa kwetu.

Tayari tunao mpango na tumeanza kusambaza mitungi ya gesi hadi vijijini, ambako tunataka mama wa kijijini atumie gesi aachane kabisa na mahangaiko ya kutafuta kuni.

Tunafahamu katika baadhi ya mikoa, moshi unaotokana na kuni umekuwa chanzo cha mauaji kwa akina mama wazee wanaokuwa na macho mekundu kwa sababu ya moshi huo wakituhumiwa uchawi. Sisi tunaamini tukimuunga mkono vyema Rais Samia tukahamasisha matumizi ya gesi vizuri, watu wetu watapata faida kubwa.”

Waziri Biteko anasema zipo faida nyingi unapotumia gesi, ambazo kati yake kubwa ni ulinzi wa misitu yetu na hivyo kuliepusha taifa na dunia na hatari ya jangwa.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko, akizungumza wakati akifungua mkutano wa 13 wa kitaaluma wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) uliofanyika Dodoma, ukiwa na kauli mbiu isemayo;
“Uandishi wa Habari Kuhamasisha Matumizi ya Gesi Kulinda Misitu

“Tunapokata misitu, tunaharibu ardhi. Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 16 ya ardhi ya nchi yetu imeharibiwa kutokana na ukataji miti holela,” anasema.

Anaongeza kuwa Ripoti ya Tatu ya Hali ya Mazingira nchini ya Mwaka 2019, inaonesha kuwa kasi ya uharibifu wa misitu ni kubwa na kila mwaka zaidi ya hekta 469,420 huharibiwa kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa.

Anafafanua kwamba hadi kufikia 2015, uzalishaji wa mkaa duniani ulikadiriwa kuwa tani milioni 52 kwa mwaka, na kati ya hizo tani milioni 32.4 zinazalishwa Afrika, ambapo asilimia 42 ya tani hizo zinazalishwa katika ukanda wa Afrika Mashariki unaohusisha nchi za Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi. Afrika Magharibi inazalisha asilimia 32, Afrika ya Kati (12.2), Kaskazini (9.8) na Kusini mwa Afrika ni asilimia 3.4.

“Takwimu hizi zinaashiria hatari kubwa. Misitu inateketea katika ukanda wetu.

Wahariri fanyeni jambo. Ungeni mkono juhudi za serikali, vinginevyo kama tusipofanya kitu, nchi yetu itageuka jangwa si muda mrefu na kwa hakika sisi kama Serikali, hatutakubali hili litokee,” anasema Biteko.

Anasema Katika Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDG) ya Mwaka 2030, Lengo Na. 7 linaelekeza upatikanaji wa nishati safi na ya bei nafuu. Sisi hapa Tanzania tumebahatika kuwa na gesi ya kutosha. Ndiyo maana, Rais Samia amesema tuitumie gesi hii, ambayo ina bei nafuu tuokoe misitu na maisha ya kina mama huko vijijini.

Hili la kutumia gesi kama nishati ya kuendeshea magari, sisi kama Wizara tunalipa msukumo mkubwa. Tunajipnaga kujenga vituo vikukbwa vya kusambaza gesi ya magari na Kanuni imeruhusu sasa wenye vituo vya mafuta vya kawaida kuongeza uuzaji wa gesi, hii tukiamini itasaidia kuongeza kasi ya kusambaza gesi ya magari nchini.

Waziri wa Habari na Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye anakiri kuguswa na kaulimbiu ya Mkutano huo, akisema.

” Sote tunafahamu kuwa Rais Samia amechaguliwa kuwa Kinara wa Uhamasishaji wa Matumizi ya Gesi Barani Afrika.

Nami nisema kaulimbiu hii imenigusa na nimefurahishwa na nia ya Jukwaa la Wahariri Tanzania kuamua kwa dhati kuunga mkono matumizi ya gesi ya kupikia majumbani.

Najua hili utalizungumzia kwa kina, lakini binafsi niwaombe wahariri katika mwaka huu wa Kitaaluma mnaouanza leo, basi tuone habari nyingi zinazoeleza faida ya matumizi ya gesi.

Tuwaondoe watu hofu juu ya matumizi ya gesi, na kubwa kama mlivyosema, tuokoe misitu yetu,” anasema Nape.

Kwa upande wake wa Kampuni ya Oryx Gas, kwa kutambua umuhimu wa wanahabari katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, iliamua kuwakabidhi mitungi ya gesiya kilo 15 pamoja na jiko lenye plate mbili, ikiwa ni sehemu ya kuwahamasisha wawe mabalozi ya kuhamasisha matumizi ya gesi.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Oryx, Benoite Araman, akizungumza na wahariri pamja na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wiki hii mtungi wa gesi wenye kilo 15 ukiwa na jiko lenye plate mbili kwa kila mhariri na waandishi wa habari kwa lengo la kuhamasisha kwa vitendo wanahabari kuunga mkono kwa vitendo kampeni ya Rais Samia ya kuhamasisha matumizi ya gesi safi ya kupikia.

Kampuni hiyo inasisitiza kuendelea kuunga mkono kwa vitendo dhamira ya Rais Samia kwa kufanikisha ndoto yake ya kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2032.

Katika kuunga mkono jitihada hizo Kampuni hiyo imekabidhi mtungi wa gesi wenye kilo 15 ukiwa na jiko lenye plate mbili kwa wahariri na waandishi wa habari kwa lengo la kuhamasisha kwa vitendo kampeni hiyo ya Rais Samia ili jamii ione haja ya kutumia ishati safi ya kupikia.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Oryx, Benoite Araman, akizungumza juzi anasema tukio hilo wamelipa uzito mkubwa na hii inatokana na umuhimu weo (wanahabari) katika jamii yetu.

“Kwetu sisi Oryx vyombo vya habari vimekuwa daraja na kuunganishi kikubwa cha kufikisha taarifa zinazohusiana na nishati safi ya kupikia na hasa inayotokana na gesi ya oryx kwa jamii.

Sote tunafahamu Serikali yetu ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Rais Samia, imeweka kipaumbele katika kuhamasisha nishati safi ya kupikia na Oryx Gas kwa kutambua umuhimu wa nishati safi tumeamua kuibeba kampeni hii kwa ukubwa wake.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Orxy Gas, Benoit Araman, akiwa kwenye picha ya pamoja na wahariri na waandishi wa habari mara baada ya kuwakabidhi majiko na mitungi wa gesi ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono kampeni ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhamasisha matumisi ya nishati safi ya kupikia. Hafla hiyo ilifanyika jana jijini Dar es Salaam.

Anasema Rais Samia ameeleza dhamira yake ni kuona ifikapo mwaka 2032 asilimia 80 ya Watanzania iwe inatumia nishati safi ya kupikia, Oryx Gas tumedhamiria kwa vitendo kufanikisha ndoto ya Rais Wetu.

“Tumekuwa tukigawa mitungi ya gesi na majiko yake bure kwa makundi mbalimbali yakiwemo ya baba na Mama Lishe,watumishi wa sekta ya afya na wajasiriamali,” anasema.

Anasema wana furaha ya kukutana na wahariri na waandishi wa habari katika tukio hilo la kuwakabidhi mtungi wa gesi wenye kilo 15 ukiwa na plate zake mbili.

“Kwetu tunakabidhi mitungi hii tukiamini ninyi ni kundi lenye ushawishi mkubwa hivyo mtasaidia kuhamasisha kwa vitendo jamii kuona haja ya kutumia nishati safi.

Mmekuwa mkishiriki katika matukio mbalimbali yanayohusu Oryx hasa katika kampeni yetu ya kuhamasisha nishati safi na katika siku hii ya leo tunasema tunawashukuru waandishi wote wa habari pamoja na vyombo vya habari mnavyofanyia kazi kwa ushirikiano wenu na mitungi hii tunayokabidhi leo ni ishara ya kurudisha shukrani zetu kwenu,” anasema Araman.

Aidha, Araman anasema wanafungua mlango wa kuhamasisha waandishi wa habari kote nchini kutumia nishati safi na hatimaye kufikia lengo la Rais Samia.

Oryx Gas Tanzania mpaka sasa imeshatoa mitungi ya gesi zaidi ya 33,000 maeneo mbalimbali nchini na kiasi cha bilioni 1.5 kimeshatumika.”Tunaahidi kama ambavyo tumekuwa tukiahidi siku zote tutaendelea na kampeni hiyo kadri ya uwezo Wetu,” anasema.

Anasema kuna faida nyingi za kutumia nishati safi na hizi ni baadhi tu:-

Anasema kwa kutumia gesi ya Oryx kwenye taasisi mbalimbali, inasaidia kuongeza ufanisi katika uzalishaji na kupunguza muda wa taasisi husika kutafuta nishati nyingine kama kuni na mkaa.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Orxy Gas, Benoit Araman, akimkabidhi mmoja wa waandishi wa habari mtungi wa gesi wa kilo 15 na plate mbili, ikiwa ni sehemu ya kuwahamasisha ili kuunga mkono kampeni ya Rais Samia ya kuhamasisha matumisi ya nishati safi ya kupikia. Hafla hiyo ilifanyika jana jijini Dar es Salaam juzi.

“Tukipika kwa kutumia Oryx Gas tunalinda mazingira yetu kwa kutokomeza ukataji wa miti, kwani misitu ni muhimu kwa kudumisha viumbe hai, kuhifadhi udongo, kusaidia mizunguko wa maji na pia uharibifu wa misitu ina haribu mifumo ya ekolojia na rasilimali za asili,” anasema.

Pia, anasema ina saidia kulinda afya ya wanawake ambao wanaathirika kwa moshi inayotokana na mkaa na kuni.

Moshi una chembe chembe za sumu ambazo husababisha magonjwa kama pneumonia, cancer ya mapafu na matatizo ya upumuaji.

Aidha, anasema inaepusha wamama na watoto kuumia kwa kubeba kuni nzito na kuepuka kujeuriwa na Wanyama wakali wakiwa wanatafuta kuni. Na wanawake wataweza kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo.

“Naendelea kuwahimiza ndugu Wahariri na Waandishi wa Habari kuendelea kuwashawishi wananchi wenzetu kupitia vyombo vya Habari, kuacha kutumia nishati chafu na kutumia zaidi nishati safi ya kupikia,” anasema.