Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Mwarobaini wa kutokomeza ukatili wa kijinsia ni kutoa taarifa hivyo wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali mkoani hapa wametakiwa kukataa utumwa wa vitendo hivyo kwa kutoa taarifa dhidi ya vitendo hivyo.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ngusa Samike,wakati akizungumza kwenye mdahalo kuhusu umuhimu wa afya ya uzazi na kupinga vitendo vya ukatili kwa ustawi wa vijana na maendeleo ya taifa ilioandaliwa na shirika la Wadada Solutions on Gender Based Violence na kushirikisha wanafunzi kutoka chuo cha SAUT,CBE,Mipango na TIA uliofanyika katika chuo cha SAUT jijini Mwanza.
Samike amewaeleza wanafunzi hao kuwa wanapaswa kuvunja mnyororo wa kufanyiwa ukatili na kutoka kwenye utumwa wa vitendo hivyo kwa kutoa taarifa ili waweze kupata msaada ambapo wakishindwa kupata msaada shuleni basi ofisi za serikali zipo wafike na kutoa taarifa dhidi ya vitendo hivyo vya ukatili.
Ameleeza kuwa vitendo hivyo vimekithiri na kwamba wanafunzi wengi vyuoni hawapati alama wanazositahili kwani ukatili unaathiri zaidi kisaikoloji kulingana na vitendo ambavyo mtu au mtoto anatendewa kutoka kwa ndugu au mtu yeyote ambaye anamfanyia ukatili.
“Zipo kesi kadhaa za ukatili wa kijinsia kwa watoto wadogo ambazo kama Mkoa tunazifuatilia,niwaombe mnapofanyiwa ukatili msipuuzie kutoa taarifa hii imekuwa kawaida mnapofanyiwa ukatili mnakaa kimya hata kama majirani wameshuhudia nao wananyamaza, nitofauti na nchi za wenzetu ambapo mtu anapofanyiwa ukatili anachukua hatua haraka kwenda kuripoti,”ameeleza Samike.
Sanjari na hayo Samike amewasihi vijana kujitambua na kutofanya maamuzi ambayo yanaweza kuleta athari kwenye jamii na kuharibu kesho yao hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha analinda afya yake kwa manufaa yake na taifa.
Mkurugenzi wa shirika la Wadada Solution on Gender Based Violence, Lucy John ameeleza kuwa katika kukabiliana na vitendo vya ukatili wanatoa elimu kuhusu afya ya uzazi na stadi za maisha kwa wanafunzi wa ngazi mbalimbali zikiwemo za msingi hadi vyuo.
“Kwenye kipengele cha elimu ya ukatili wa kijinsia, shirika linatoa elimu kwa wanafunzi kubaini viashiria vinavyoashiria vitendo hivi ni dalili ya ukatili lakini kwa upande wa vyuo tunatoa elimu waweze kujua kijikinga na vitendo hivyo,” amesema Lucy.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha Saut-Taaluma Profesa Hosea Rwegoshora , amewasihi vijana kuzingatia elimu inayofundishwa shuleni ili iwasaidie katika vizazi vijavyo.
“Shida kubwa iliyopo kwa sasa ni vijana kuzaliwa kipindi ambapo utandawazi umezidi hivyo kijana hapati elimu ya afya ya akili na uzazi kwa kiwango kile ambacho watu wa zamani walikuwa wanapata, siku hizi utandawazi umekuwa ndio elimu yao kuu na vijana wengi hawazingatii tena maadili na maelekezo ya wazazi wao,”amesema Prof.Hosea.
Mratibu wa Afya ya Uzazi Halmashauri ya Jiji la Mwanza Bertha Yohana,amesema kukosekana kwa elimu ya afya ya uzazi kunaweza kuchangia ukatili wa kijinsia kwani anakuwa hana elimu ya stadi za maisha ambayo itamsaidia kuwa na mbinu mbalimbali za kujikinga na ukatili.
Hivyo amesema kama serikali wanajitahidi kutoa elimu zaidi na kuhakikisha wanawajengea uwezo vijana ili waweze kuwa na utambuzi na stadi za maisha ambazo zitawasaidia kujilinda na ukatili katika maisha yao.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu