Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
WANAFUNZI wa shule ya Msingi na Sekondari ya East Africa ya Dodoma jana Jumamosi walikonga nyoyo za wageni waalikwa baada ya kuonyesha vipaji vya hali ya juu kwenye kuzungumza lugha tatu kwa ufasaha.
Lugha hizo tatu ni Kingereza, Kifaransa na Kichina.
Wanafunzi hao walionyesha umahiri wa hali ya juu kwenye kuzungumza kwa ufasaha lugha ya kiingereza, Kifaransa na kichina walipokuwa wakiwasilisha masuala mbalimbali ya kitaaluma.
Wanafunzi hao walionyesha umahiri kwenye kuelezea masuala mbalimbali ya kitaaluma kwa kutumia lugha ya kingereza fasaha, Kifaransa na kichina hali ambayo iliwafanya wazazi waliohudhuria mahafali hayo kulipuka kwa shangwe .
Mgeni rasmi kwenye mahafali hayo alikuwa Kaimu Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma, Prisca Myala ambapo pia mahafali hayo yalihudhuriwa na wageni mbalimbali akiwemo Mkurugenzi wa shule za St Mary’s na East Africa ya Dodoma, Dk. Rose Rwakatare.
Mmoja wa wazazi aliyehudhuria mahafali hayo yanayoendelea, Mtaita Salum alisema uwezo wa wanafunzi hao unaonyesha namna walivyoandaliwa vyema na walimu mahiri.
“Kuzungumza Kifaransa na kingereza kwa ujasiri namna ile ni jambo ambalo limenifurahisha sana kwa kweli na tunajua umuhimu wa lugha za kigeni duniani kwa hiyo badala ya kukazania kingereza tu ni vyema tukaiga hawa wenzetu East Africa kuwafundisha wanafunzi lugha zingine kama kichina,” alisema
Alisema pia amefurahishwa kuona namna wanafunzi wa shule hiyo walivyoonyesha umahiri wa kuelezea masuala ya kitaalamu.
Mzazi mwingine, Abdul Hamza, alisema amefurahi sana kuona wanafunzi wa shule hiyo wanajiamini katika kuzungumza lugha zote kwa ufasaha na bila kubabaika.
“Wamemudu sana kuelezea masuala mbalimbali ya kitaaluma na unaweza ukadhani kwamba ni watu ambao wako kazini kutokana na umahiri wao nawapongeza sana walimu wa East Africa ya hapa Dodoma kwa kufanyakazi usiku na mchana kupata mafanikio haya,” alisema
Mkurugenzi wa shule hiyo, Dk. Rose Rwakatare alisema uongozi wa shule utaendelea kuboresha miundombinu mbalimbali ili kuhakikisha shule inaendelea kuongoza kitaaluma mkoa wa Dodoma.
Alisema kwenye mitihani ya utahimilifu mwaka huu shule hiyo imekuwa ya tatu na kwamba kuanzia mwakani watahakikisha wanakuwa namba moja kwani wamepanga kufanya maboresho makubwa ya miundombinu na ufundishaji.
Alisema kwa maandalizi mazuri yaliofanywa kwa wanafunzi wa darasa la saba mwaka huu ana uhakika wanafunzi wote watafaulu kwa alama A na wengine kuingia kwenye nafasi ya 10 bora kitaifa.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best