November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanafunzi NIT walivyobuni mashine za kuwasaidia wakulima ,wafugaji

Mashinemashine ya kuchanganya chakula cha mifugo ambayo kukoboa na kusaga kwa wakati mmoja na mashine ya kutengeneza siagi na kutoa mafuta kwa wakati mmoja.
mashine ya kufugia vifaranga vya kuku mara baada ya kutotolewa ili viweze kuwa salama dhidi ya ndege na wanyama kama paka,panya na mbwa.

Na Joyce Kasiki,Dodoma

CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimekuja na Teknolojia za kilimo na ufugaji kwa ajili ya kumrahisishia mkulima kutumia nyenzo rahisi za uchakataji mazao.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la Chuo hicho,Mwalimu aliyeambatana na wanafunzi waliotengeneza bunifu hizo Mhandisi Kelvin Odhiambo amesema, wamekuja na wanafunzi wao ili kuonesha bunifu wanazotengeneza kwa sababu zinawahusu na zinaweza kuwasaidia wakulima.

Amesema, wanafunzi hao wametengeneza mashine za kuchakata vyakula mbalimbali , mashine ya kusambaza mbolea na mashine ya kufugia vifaranga vikiwa bado vidogo.

Amewaasa vijana na wananchi kwa ujumla wenye sifa kujiunga na chuo hicho ili waweze kupata ujuzi wa bunifu mbalinbali.

“Tayari NIT imefungua dirisha la usaili kwa ngazi ya stashahada na shahada ,waliomaliza kidato cha nne na cha sita wanakaribishwa kujiunga na chuo hicho.”amesema Mhandisi Odhiambo

Mwanafunzi wa chuo hicho George Valentine amesema ametengeneza mashine ya kufugia vifaranga vya kuku mara baada ya kutotolewa ili viweze kuwa salama dhidi ya ndege na wanyama kama paka,panya na mbwa.

“Mashine hii ni nzuri kwa kufugia vifaranga,baada ya kuzaliwa na kupewa chanjo,vifaranga vinatunzwa katika mashine hii na vinakuwa salama dhidi ya panya,ndege na wanyama wanaokula vifaranga lakini pia vinapata joto linalohitajika pamoja na chakula na maji kwa wakati unaohitajika.”amesema George

Amesema mashine hiyo ina uwezo wa kutoa taarifa pale chakula na maji vinapopungua.

Naye Omary Athumani mwanafunzi wa chuo hicho amesema amekuja na mashine ya kuchanganya chakula cha mifugo ambayo kukoboa na kusaga kwa wakati mmoja na mashine ya kutengeneza siagi na kutoa mafuta kwa wakati mmoja.

“Mashine hii ina uwezo wa kutengeneza bidhaa husika kwa kilo 100 kwa saa moja.”

Amesema,ametengeneza mashine hizo ili kumsaidia mkulima dhidi ya mazingira magumu ambayo anapitia kwani kupitia mashine hiyo mkulima anaweza kuchakata mazao yake na kuuza mazao yaliyochaktwa na kupata faida badala ya kuuza mazao ghafi.

“Kwa hiyo kwa ujumla bidhaa tunazobuni na kuzitengeza,ni bidhaa ambazo zimelenga kutatua changamoto katika jamii.”amesisitiza Omary