November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanafunzi waishio katika mazingira magumu wapewa msaada

Na Mwandishi Wetu.

WANAFUNZI 51 wanaotoka kwenye familia duni waliochaguliwa kujiunga na sekondari kidato cha kwanza mwaka huu kutoka kata tatu za Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha wamepewa msaada vifaa na mahitaji mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya Sh.Milioni 12 ili kuwawezesha kwenda shule.

Vifaa walivyokabidhiwa wanafunzi hao ni pamoja na magodoro, tranka,sare za shule,sabuni, taulo za kike, viatu, mikebe,mashuka,madaftari,kalamu,ndoo,limu, ‘toilet paper’ ambavyo vilichangwa na wadau mbalimbali wa maendeleo kusaidia wanafunzi waweze kuendelea na masomo ya sekondari.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Ngorongoro, Mohamed Bayo alimaarufu Marekani amesema wanafunzi waliopata msaada huo wanatoka katika familia duni kutoka kata za Orgosorock, Enguserosambu na Oloirien.

Bayo akizungumza baada ya kukabidhi vifaa hivyo amewataka wanafunzi hao wa kike wasiende kurubuniwa kwa mapenzi hali itakayowafanya washindwe kuendelea na masomo.

“Nyie mnatoka katika familia ambazo zina changamoto hivyo mnatakiwa mkasome kwa bidii ili baadaye mje msaidie wazazi wenu,” amesema.

Amesema utaratibu wa kusaidia wanafunzi wanaotoka katika familia duni umeanza tangu 2021 baada ya kuanzishwa kwa mfuko maalum wa diwani wa kata ya Orgosorock.

Bayo ambaye pia ni Diwani wa kata ya Orgosorock amesema mfuko huo tangu umeanzishwa umesaidia jumla ya wanafunzi 104 waliochaguliwa kujiunga na shule za sekondari za serikali na kiasi cha zaidi ya Sh.Milioni 24 kimeshatumika.

Ameongeza kuwa mfuko huo ambao pia unaundwa kwa kushirikisha viongozi wa dini mbalimbali, malengo ni kutaka kuufanya uwe mfuko wa wilaya ambao utawawezesha wanafunzi wote wanaotoka familia duni katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro waweze kunufaika.