November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanafunzi waaswa kusoma masomo ya sayansi

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe

WANAFUNZI wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne wametakiwa kusoma masomo ya sayansi ili kukabiliana na mwendokasi wa Sayansi na Teknolojia katika ulimwengu wa utandawazi.

Lakini pia wametakiwa kusoma kwa bidii, kwani hakuna njia ya mkato katika kupata mafanikio na nchi ya Tanzania inakwenda kwenye uchumi wa viwanda na ajira binafsi, hivyo wasiposoma kwa bidii, watashindwa kukabiliana na changamoto za dunia.

Hayo yamesemwa Agosti 31, 2024 na Meneja wa Tume ya Kikristo ya Huduma za Kijamii Kanda ya Mashariki (CSSC) Diana Leonard. Ni kwenye mahafali ya 26 ya darasa la awali, mahafali ya 19 ya darasa la saba, na mahafali ya 13 ya kidato cha nne. Shule hizo zipo chini ya Taasisi ya Rock Memorial Education Trust (RMET) mjini Korogwe.

“Hakuna njia ya mkato katika maisha, someni kwa bidii ili muendelee kuiweka shule hii katika nafasi ya kwanza kiwilaya na kimkoa. Zingatieni kuwa Serikali yetu inasisitiza masomo ya sayansi ili kukabiliana na mwendokasi wa teknolojia na utandawazi duniani. Hivi sasa nchi yetu inaelekea katika uchumi wa viwanda na ajira binafsi katika sekta mbalimbali” amesema Leonard.

Leonard aliwataka wazazi kuwapa moyo watoto wa shule za awali, kwani elimu ya awali ndiyo kichocheo cha kuendeleza elimu na taaluma zote duniani, huku akiwaeleza wanafunzi wa darasa la saba kuwa elimu ya msingi ni moja ya ngazi ya kuelekea kwenye elimu, hivyo waweze kuendelea kuwa watulivu, na kujenga nidhamu kwa wazazi na walimu ili wapate elimu ya juu kama watangulizi wao.

“Hii imejidhihirisha kwa maelezo niliyopata kuwa vijana wote waliosoma hapa Hills View English Medium School, miongoni mwao sasa wana shahada mbalimbali wakihudumia Taifa, na wengine wako nje ya nchi. Nawapongeza sana vijana hao na kuwaombea waendelee kusonga mbele.

“Bila shaka, hata ninyi ni mashuhuda kuwa wazazi wenu wanafanya kila jitihada kujitoa kwa hali na mali kuwalipia ada zote mnazozihitaji, kuwatia moyo katika safari yenu hii ya kutafuta elimu wakishirikiana bega kwa bega na walimu wenu wa shule. Hivyo, nawaasa kuwa endeleeni kupambana na changamoto zozote zinazojitokeza ili muweze kutimiza wajibu wenu kwa wazazi, familia na Taifa kwa ujumla” amesema Leonard.

Awali, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Hills View Charles Mhuza, amesema shule hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1999 imekuwa ikifanya vizuri kwa kushika nafasi ya kwanza na ya pili kiwilaya, lakini pia kufanya vizuri kimkoa na kitaifa.

“Wahitimu wa kiume wa darasa la saba wakiingia ukumbini.”

“Msingi imara uliwekwa na walimu na wanafunzi waanzilishi wa shule hii, umefanya kila waliofuata kutaka kuvunja rekodi ya waliotangulia. Hii imefanya shule hii kukamata nafasi ya kwanza na pili kwa mfululizo kiwilaya. Vile vile, mwaka huu katika mitihani ya majaribio kimkoa na kiwilaya, wameshika nafasi ya kwanza kiwilaya, na nafasi ya 11 kimkoa.

“Vijana waliomaliza darasa la saba hapa miaka ya nyuma, wote wamemaliza vyuo vikuu hapa nchini, na wengine huko India, Uganda, na Ujerumani, na sasa wana taaluma mbalimbali, wapo madaktari, wahandisi, wahasibu na marubani. Siri ya mafanikio haya yamesababishwa na usikivu wa watoto, mazingira tulivu ya kujifunza, afya bora na lishe, na mshikamano wa wafanyakazi wote ambao hufanya kazi kwa pamoja” amesema Mhuza.

“Mkurugenzi Mtendaji wa RMET Sylvester Mgoma (kulia) akimuongoza mgeni rasmi wa mahafali hayo Diana Leonard (wa pili kulia) kuingia ukumbini.”

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Hill View Prackiseda Makame amesema wanafunzi wanaojiandaa na mitihani ya kidato cha nne wamesema wapo tayari kukabiliana na mitihani hiyo, na wameahidi kufanya vizuri kwenye mitihani hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya RMET Sylvester Mgoma, ambayo ipo chini ya Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga, na  ndiyo inamiliki shule ya awali, msingi, sekondari na chuo cha kati, amesema ameimarisha mifumo ya ufanyaji kazi kwenye taasisi hiyo kuanzia shule ya awali hadi chuo kwa ile Filosofia ya kufanya kazi kwa bidii, ili kuanzia wanafunzi, walimu na wafanyakazi, kila mmoja awajibike pale alipo, ndipo maendeleo ya pamoja yatafikiwa.

“Wahitimu wa kike wa kidato cha nne wakiingia ukumbini.”