Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online DSM
WANAFUNZI wa shule ya St Mary’s Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, wameibuka kidedea kwenye shindano la kujibu maswali mbalimbali yanayohusu kodi.
Shule hiyo iliibuka nafasi ya pili ikitanguliwa na shule ya sekondari ya Kibaha mkoani Pwani katika shindano hilo lililofanyika kwenye Chuo cha Kodi Mikocheni.
Shindano hilo lililodumu kwa siku tatu liliendeshwa hivi karibuni na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kushirikisha shule 59 za sekondari binafsi na za umma.
Akizungumzia shindano hilo jana, Mwenyekiti wa bodi ya shule hizo, Dallas Mhoja alisema kufuatia ushindi huo wanafunzi wa shule hiyo walizawadiwa kompyuta, mashine ya kudurufu, kombe na medali mbalimbali.
“Huwa tunashiriki mashindano mbalimbali yanayoandaliwa na TRA kwa hiyo mwaka huu tumeshiriki zilikuwa shule 59 na katika hizo shule tulibuka washindi wa pili nyuma ya Kibaha iliyokuwa ya kwanza,” alisema
Aidha, alisema tukio hilo limefanywa na taasisi kubwa ya serikali kwa kushirikisha shule binafsi na za serikali hivyo ushindi wa shule hiyo ni jambo la kujivunia kwa uongozi mzima wa shule.
Alisema wanafunzi wa shule hiyo walionyesha umahiri wa hali ya juu katika kujibu maswali mbalimbali yanayohusiana na kodi hali iliyowafanya kuibuka wa pili.
“Kushindana na shule 59 za Mkoa wa Dar es Salaam, zikiwemo za binafsi na za serikali na kuibuka kwenye nafasi ya pili tunaona siyo jambo dogo kwetu. Tunajivunia mafanikio haya na mashindano yajayo tutashika namba moja,” alisema
Alitaja siri ya mafanikio hayo kuwa ni maandalizi mazuri ya wanafunzi na walimu wenye kuipenda kazi yao ambao wamekuwa wakifanya kazi usiku na mchana.
“Shindano hili limeleta msisimo mkubwa sana kwa wanafunzi wetu na walimu walioshiriki kwasababu mbali na zawadi kama kompyuta walizawadiwa fedha taslim kwa hiyo mashindano haya ni muhimu sana,” alisema
More Stories
Wanafunzi 170 wapata ufadhili wa masomo
Maelfu kunufaika namsaada wa kisheria Katavi
Serikali yazidi kuwakosha wawekezaji wadau waipa tano