Na Rose Itono,Timesmajira, Online
NAIBU Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Profesa Richard Kangalawe amewataka wanafunzi wa chuo hicho kuhakikisha wanapima afya zao, ili waweze kujikinga na kuwalinda wengine kutokana maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI ya chuo hicho Dar es Salam jana Profesa Kangalawe amesema kuna kila sababu ya wanafunzi kuwa na elimu ya kutosha kuhusiana na masuala ya UKIMWI, ili wawe mabalozi wazuri kwa wengine.
“Acheni tabia ya kupimana kwa macho, badala yake kuweni na utaratibu wa kuwaona wataalamu wa afya kwa ajiili ya kujua hali zenu, ili kuepuka unyanyapaa,” amesisistiza.
Kwa upande wake Mratibu wa Maadhimisho hayo ambaye pia ni mshauri wa wanafunzi chuoni hapo, Ukende Mkumbo amesema siku hiyo ni muhimu na ipo kimkakati hasa katika kipindi hiki, ambacho wanafunzi wanaelekea kwenye mafunzo kwa vitendo (field) na likizo itawawezesha kujikinga, kuwalinda wengine na kusaidia serikali kuwa na nguvu kazi imara.
Kwa upande wake Ofisa kutoka Ofisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU ) Wilaya ya Kigamboni, Neema Kilongozi amesema taasisi hiyo ina mahusiano ya moja kwa moja katika kupiga vita maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi kwa wanafunzi, hususan rushwa ya ngono.
Nao baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho akiwemo Rais wa Serikali ya Wanafunzi, Godson Munisi na Makamu wake Hafsa Sheturi, wamesema mafunzo waliyoyapata kuhusiana na elimu ya UKIMWI ni chachu katika nyanja mbalimbali za kijamii, kisiasa, kiuchumi na itawawezesha kuwa mabalozi wazuri kwa kujikinga na kuwakinga wengine.
More Stories
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM