January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanafunzi 93,000 Jijini Mbeya kupatiwa vyandarua bure

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

ZAIDI ya wanafunzi 93,000 wa shule za msingi katika halmashauri ya jiji la Mbeya wanatarajia kupewa vyandarua bure ikiwa ni mkakati wa serikali wa kutokomeza ugonjwa wa Maralia nchini.

Akitoa taarifa leo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kugawa vyandarua kwa shule za msingi jijini Mbeya, mganga wa jiji Dkt. Yesaye Mwasubila amesema zoezi hilo la siku tatu litazihusisha shule za msingi 105 zilizopo halmashauri ya jiji la Mbeya.

Amesema jumla ya vyandarua 93,399 vitatolewa bure kwa wanafunzi wa shule za msingi kuanzia darasala la awali hadi la sita na kwamba miongoni mwa shule hizo zipo za umma na binafsi.

“Zoezi hili linafanywa na serikali kupitia ofisi ya Rais Tamisemi na wizara ya afya lakini waliopewa jukumu la kusambaza vyandarua hivi ni bohari ya dawa ya serikali (MSD), na lengo hasa la kampeni hii ni kuongeza mapambano dhidi ya ugonjwa wa Maralia’’ amesema

Naye mkuu wa wilaya ya Mbeya Beno Malisa amewasihi wanafunzi watakaopewa vyandarua hivyo kutoa taarifa kwa walimu wao endapo wataona wazazi au walezi wao wanavitumia vinginevyo ikiwemo kufugia kuku na kuweka uzio wa bustani.

Amesema wapo baadhi ya watu kwenye jamii wanatumia vyandarua vinavyotolewa na serikali kinyume na maelekezo kitendo alichokitaja kuwa kinakwamisha kwa makusudi jitihada za serikali za kukabiliana na ugonjwa wa Maralia.

Aidha, amewakumbusha waalimu umuhimu wa kuwafundisha watoto jinsi ya kutumia vyandarua hivyo kwa ufasaha ili kuwezesha lengo kuu la serikali la kutokomeza maralia nchini litimie kikamilifu.

Afisa uhusiano wa bohari ya dawa nchini (MSD), Samwel Kamugisha amesema wamejipanga kuhakikisha zoezi la kusambaza vyandarua linafanyika kwa ufanisi kwani wana wataalam wa kutosha pamoja na vitendea kazi.