December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

WanaCCM 51 wachukua fomu kugombea uenyekiti Tabora

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

WANACHAMA 51 wa Chama Cha Mapinduzi wamechukua fomu ya kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa huo Mzee Hassan Mohamed Wakasuvi aliyefariki dunia Februari 21 mwaka huu.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa, Idd Moshi amesema kuwa jumla ya wanaCCM 51 kutoka maeneo mbalimbali wamechukua fomu kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi hiyo.

Amesema kuwa zoezi la uchukuaji fomu lilianza Aprili 6, 2024 na kumalizika jana Aprili 8, 2024 saa 10.00 jioni ambapo hadi dirisha linafunguwa jumla ya makada 51 wamejitokeza kuchukua fomu na kati yao 4 hawakurejesha fomu zao.

Mwenezi amefafanua kuwa kati ya makada 51 waliochukua fomu 45 ni wanaume na 6 ni wanawake na miongoni mwao ni Viongozi wa Chama katika ngazi mbalimbali, viongozi wa serikali na wanachama wa kawaida.

‘Zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora limekamilika, sasa tunaingia hatua nyingine ya usaili wa awali, kupitia fomu za wagombea wote’, alisema.

Idd amebainisha kuwa Aprili 11, 2024 Kamati ya Usalama na Maadili ya Chama ngazi ya Mkoa itakutana ili kupitia majina ya wagombea wote, baada ya hapo Aprili 13, 2024 Kamati ya Siasa ya Mkoa itakutana na kutoa mapendekezo yao.

Ameongeza kuwa baada ya mchakato wa awali wa vikao vya Chama ngazi ya Mkoa, majina ya wagombea waliopendekezwa yatapelekwa Makao Makuu ya Chama ili kuendelea na mchakato mwingine ikiwemo uteuzi wa mwisho wa wagombea.

‘Uchaguzi ndani ya CCM ni wa kidemokrasia, kila mgombea ana haki sawa na mwenzake, naomba wagombea wote na wanaCCM tuendelee kuwa watulivu hadi vikao vya vyuu vitakapofanya uteuzi wa mwisho na kutuletea majina’, amesema.

Aidha Mwenezi amewataka wagombea wote kutofanya kampeni ya aina yoyote ile katika kipindi hiki hadi watakapoletewa majina na kutangazwa utaratibu wa uchaguzi huo ikiwemo tarehe ya uchaguzi na siku ya kuanza kampeni.

Ameonya kuwa chama hakitasita kumchukulia hatua mgombea yeyote atakayefanya kampeni kinyume na utaratibu na jina lake linaweza kuondolewa katika orodha ya wagombea.