Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
WAJUMBE wa Baraza la Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoani hapa wametoa tamko la kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan za kuwaletea maendeleo Watanzania.
Akitoa tamko katika kikao cha Baraza hilo kilichofanyika jana, Mwenyekiti wa UWT Mkoa Mwanne Mchemba alisema Rais amedhamiria kuinua uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla kupitia uwekezaji katika bandari ya Dar es salaam.
Alibainisha kuwa ukosoaji unaoendelea sasa juu ya dhamira ya serikali kuingia makubaliano na Kampuni ya DP World kuwekeza katika bandari hiyo hauna tija kwa kuwa dhamira ya Rais ni kuboresha utendaji wa bandari hiyo, kuleta ufanisi na kuongeza mapato.
Alisisitiza kuwa Mama anajali sana ustawi wa wananchi wake ndiyo maana ameendelea kumwaga mabilioni ya fedha katika halmashauri zote nchini ili kufanikisha utekelezaji miradi mbalimbali ya maendeleo.
‘Kwa niaba ya Wajumbe wote wa Baraza la UWT Mkoa, natoa tamko la kuunga mkono juhudi zote zinazofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan za kuwaletea maendeleo wananchi na taifa kwa ujumla’, alisema.
Mchemba aliongeza kuwa wako pamoja na Mheshimiwa Rais na wataendelea kusimama imara na kuyasema kwa dhati yale yote anayoyafanya ili jamii ielewe dhamira yake na kutowapa nafasi wapotoshaji wanaopitapita mitaani.
Awali akitoa salamu za chama katika mkutano huo Katibu Msaidizi wa CCM Mkoa Mwita Nakururu aliwataka wana UWT wote kushikamana na kuendelea kuyasema mazuri yote yanayofanywa na Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alibainisha kuwa Mheshimiwa Rais anataka kuona bandari ya Dar es salaam ikiendeshwa kisasa na kuwa chanzo kikuu cha mapato ya nchi ili kufanikisha utekelezaji shughuli mbalimbali za maendeleo ya wananchi.
Alisisitiza kuwa kupitia uwekezaji huo ajira zitapatikana kwa wingi hivyo vijana na akinamama wanatanufaika kupitia fursa hiyo na kuendesha maisha yao.‘Wapuuzeni wale wote wanaobeza au kupinga dhamira njema ya serikali ya awamu ya sita ya kuingia makubaliano ya uwekezaji katika bandari hiyo ili kuongeza ufanisi wake na kuchochea uchumi wa taifa’, alisema.
Akitoa taarifa ya utekelezaji majukumu ya Jumuiya hiyo, Katibu wa UWT Mkoa Rhoda Madaha alisema wamefanikiwa kuhamasisha akinamama katika wilaya zote 7 za mkoa huo kuanzisha miradi ya maendeleo ili kujikwamua kiuchumi.
Aliwapongeza wabunge 2 wa viti maalumu wa Mkoa huo (Munde Tambwe na Jackline Kainja) kwa juhudi zao kubwa za kuwezesha akinamama wa Mkoa huo kuanzisha miradi ya kiuchumi.
Alisema juhudi hizo zimechochea kwa kiasi kubwa uhai wa Jumuiya hiyo, kuongeza wanachama na matawi yote ya UWT kuanzia ngazi za Vijiji, Kata, Wilaya na Mkoa kuwa na miradi endelevu.
More Stories
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania