November 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wampongeza Rais Samia kwa huduma za msaada wa kisheria

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline, Morogoro

WANANCHI wanaopata msaada wa kisheria za mama Samia Legal Aid zinazoendelea kutolewa kwenye maonyesho ya Nane nane mkoani Morogoro wameelezea namna walivyonufaika na huduma hizo.

Wakizungumza mkoani hapa jana, wananchi hao walimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka huduma hizo kwenye maonyesho hayo ambapo wamesema zimekuwa mkombozi kwao.

Renatha Manda alimshukuru Rais Samia kwa msaada wa kisheria baada ya kusaidiwa na huduma hizo alipokwenda kwenye maonyesho hayo.

“Nilikuwa na tatizo la mirathi nikaenda wakanipa ushauri wa kisheria na kwa kweli nimeridhika na najua suala langu litafika mwisho hivi karibuni,” alisema

Luciani Mwanitu kutoka Nzuguni Dodoma alisema alifika kwenye banda la Mama Samia Legal Aid ambapo amepata elimu kuhusu namna wanavyotoa huduma hizo na alishauri huduma hizo zipanuliwe ili wananchi wengi hasa wa vijijini waweze kufikiwa.

“Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kuanzisha huduma hii ambayo imekuwa mkombozi kwa wananchi wengi sana. Nawaomba waisogeze zaidi vijijini ili wananchi wengi zaidi waendelee kunufaika nayo,” alisema

Uwezo Maulid mkazi wa Shinyanga aliyefika kwenye banda hilo alisema amesaidiwa kwenye kesi ya mirathi ya mume wake ambaye alikuwa mtumishi wa umma kwenye manispaa ya Shinyanga Mjini.

“Nimefika hapa wamenipokea vizuri wamenipa mwanasheria wa huko Shinyanga ili aweze kunisimamia kupata haki zangu za msingi mimi mke wa merehemu Seif,” alisema na kuongeza

“Naomba mheshimiwa Rais aweze kunisaidia kwasababu kila ninapokwenda mahakamani naambiwa nirudi nyumbani mtandao umegoma kwasababu siku hizi kesi zinaendeshwa kwa mtandao. Huu ni mwaka wanne tangu mwaka 2021 nilipokonywa hadi nyumba na ndugu wa marehemu,” alisema

Alisema lakini baada ya kufika kwenye banda la mama Samia Legal Aid na kupewa mwanasheria anaamini suala lake litashughulikiwa na kufika mwisho ili aweze kupata haki zake kama mjane wa marehemu mume wake.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji Haki wa Wizara ya Katiba na Sheria, Beatrice Mpembo alisema wakati wanasheria wengine wakiwa kwenye ziara na Rais Samia kutoa msaada wa kisheria, Rais Samia ametuma wanasheria wengine kupitia Kampeni ya Mama Samia Legail Aid kutoa huduma za msaada wa kisheria kwenye maonyesho ya nane nane mkoani humo.

Beatrice alisema timu ya wanasheria hao iliwasili mkoani Morogoro wiki iliyopita na inaendelea na kazi ya kuwahudumia wananchi mbalimbali ambao wanamatatizo ya kisheia kwa kuwapa msaada wa kisheria.

Alisema tangu wanasheria hao wawasili kwenye viwanja vya nane nane mkoani Korogoro wananchi wengi wamekuwa wakifika kwenye banda la mama samia Legal Aid katika maonyesho hayoambapo wamekuwa wakipewa msaada wa kisheria.